(NDA) imekamata shehena ya L-Coffee, iliyoingizwa nchini humo kama nyongeza ya nguvu mwilini na lishe. Picha: AP. 

Mamlaka ya Uganda ya kukabiliana na mihadarati, maarufu (NDA) imetangaza kukamata shehena ya L-Coffee, iliyokuwa ikiingizwa nchini humo kama nyongeza ya lishe.

NDA imesema kwenye taarifa yake kuwa, licha ya pakiti ya L-Coffee kuonyesha kuwa ni mchanganyiko wa kahawa ya Arabica na Robusta ya kuongeza nguvu mwilini, uchunguzi wa baadhi ya vipimo vyao vinaonyesha kuwa bidhaa hiyo imechanganywa na tadalafil, dawa ya kutibu tatizo la nguvu za kiume.

"Tumeifanyia majaribio na kugundua kuwa Kahawa ya L-Power imechanganywa na Tadalafil, dawa iliyoagizwa na maagizo ya kuharibika kwa nguvu za kiume yenye madhara makubwa ikiwa ni pamoja na matatizo ya kupumua na ya moyo. Tunaagiza kwa kusimamishwa mara moja kwa uuzaji na utumiaji wa bidhaa hii" Imesema kwenye taarifa yake.

NDA sasa inawaonya raia wa nchi hiyo dhidi ya matumizi ya Kahawa aina ya L-Power ambayo kufuatia uchunguzi wake wa kimaabara, umethibitisha kuchanganywa na Tadalafil, aina ya dawa isiyostahili kutumika bila maagizo ya daktari.

"Tadalafil ni dawa ya kutibu kuharibika kwa nguvu za kiume ambayo lazima itumike chini ya maelekezo madhubuti na mtaalamu wa matibabu aliyehitimu kwani ina madhara makubwa ambayo ni pamoja na; matatizo makubwa ya kupumua na moyo, matatizo ya mkojo na wakati mwingine kusababisha kukosa fahamu na kifo." Iliongeza.

Uganda sasa imepiga marufuku uuzaji, uhifadhi, na usambazaji wa kahawa ya L-Power na kuyaonya maduka yote ya dawa, yakiwemo ya kufanya uuzaji wa bidhaa mtandaoni au wauzaji wowote wa dawa na virutubisho vya lishe kusimamisha uuzaji wa bidhaa hiyo.

Kwa sasa Mamlaka hiyo ya kupambana na dawa za kulevya, NDA, imesema itawachukulia hatua wanaohusika kwenye uingizaji wa kahawa hiyo na kuongeza kuwa imewajulisha rasmi waagizaji wa L-Power kuwajibika kikamilifu kwa uharibifu wake na kurejesha (kukusanya soko) bidhaa zozote ambazo zimeingizwa Uganda kinyemela. |"NDA, pamoja na vyombo vingine vya kutekeleza sheria vinaendelea kuchunguza suala hili ili kuhakikisha kwamba wale wanaohusika wanawajibishwa." Ilisema.

TRT Afrika