Baadhi ya wabunge wanadai mabadiliko hayo yanaweza kuvuruga utaratibu uliopo hivi sasa. / Photo: AFP

Wabunge kadhaa nchini Uganda wanapendekeza muswada wa kubadilisha mfumo wa sasa kwa kufanya nafasi ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuwa ya kuchaguliwa.

Chini ya utaratibu wa sasa, kiongozi wa upinzani anateuliwa na chama cha upinzani chenye idadi kubwa ya wabunge Bungeni.

Kiongozi wa upinzani ni nafasi muhimu ndani ya Bunge, yenye jukumu la kuteua Baraza la Mawaziri Kivuli ( shadow ministers), kuandaa na kuwasilisha bajeti mbadala, na kuhudumu kama mjumbe wa Tume ya Bunge.

Kwa kawaida, kiongozi wa upinzani anatoka chama cha The National Unity Platform, NUP kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi , msanii maarufu Bobi Wine ambaye ni mbunge.

Richard Lumu, mbunge wa Mityana Kaskazini na mwanachama wa chama cha Upinzani cha Democrtaic Party, ndiye alitoa pendekezo hilo.

Muswada wa Lumu pia unalenga kubadilisha jinsi Mnadhimu Mkuu wa Upinzani anavyochaguliwa, na kupendekeza kuwa, nafasi hii pia inapaswa kuchaguliwa na wabunge wa upinzani badala ya kuteuliwa na chama cha upinzani kilicho na wengi.

Chini ya utaratibu wa sasa, Kiongozi wa Upinzani anateuliwa na chama cha upinzani chenye idadi kubwa ya wabunge Bungeni/ Picha: Wengine

Lumu anataka Kifungu cha 8 cha Sheria ya Utawala wa Bunge kifanyiwe marekebisho ili kuruhusu wabunge wote wa upinzani kuchagua kiongozi wa upinzani, bila kujali itikadi za vyama.

Mabadiliko haya yanaweza kuvuruga utamaduni wa chama cha upinzani chenye wabunge wengi kushikilia nafasi ya kiongozi wa upinzani, na hivyo kuvipa vyama vidogo kama vile DP sauti katika uteuzi.

Lumu alitetea pendekezo lake, akilinganisha uchaguzi wa kiongozi wa upinzani na michakato ya kidemokrasia katika muktadha mwengine.

“Uchaguzi ni kielelezo cha demokrasia. Nikiwa Mkatoliki najua hata Papa amechaguliwa. Hivi kwa nini Kiongozi wa Upinzani asichaguliwe pia? Tunamchagua Spika wa Bunge, na pia tunamchagua Rais. Hakuna sababu kwa nini tusichague Kiongozi wetu wa Upinzani," Lumu aliteta.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa NUP Mbwatekamwa Kakembo, Mbunge wa Manispaa ya Entebbe, ambaye alidai kuwa mfumo wa sasa unaruhusu kiongozi wa upinzani kupendelea chama chao.

"Tumeona matukio ambapo Kiongozi wa Upinzani anakuwa kama mwakilishi wa chama chao pekee. Hii ilikuwa kweli kwa FDC, na sasa tunaiona na NUP. Tukimchagua kiongozi wetu watatuheshimu na kutuunganisha sote na kutufanya tuwe na nguvu zaidi,” Kakembo alisema.

Hata hivyo, upinzani dhidi ya mswada huo ulitolewa na baadhi ya wabunge, akiwemo Okin P.P. Ojara mbunge wa Chwa Magharibi na Denis Oneka Lit mbunge wa Manispaa ya Kitgum.

Ojara alionya kuwa mabadiliko yanayopendekezwa yanaweza kuvuruga muundo wa sasa wa Bunge, akibainisha kuwa chama tawala hakichagui vigogo wake Wakuu au Mawaziri Wakuu.

“Hii hoja kwa kweli ni hatari sana. Mpangilio wa sasa unafanya kazi vyema, na Bunge kama taasisi halijakabiliwa na changamoto zozote na kiongozi wa upinzani chini ya utawala wa sasa wa kisheria,” Ojara alisisitiza.

Spika Anita Among aliamua kuunga mkono hoja ya Lumu, akisisitiza kwamba kwamba, muswada huo haumlengi mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na kiongoiz wa upinzani wa sasa, Joel Ssenyonyi.

Spika alimuagiza Katibu wa Bunge, Adolf Mwesige, kusaidiana na Lumu katika kuandaa muswada huo kwa ajili ya kufikishwa bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza.

TRT Afrika