Jeshi la Uganda limemkamata kamanda wa kundi la waasi linaloshirikiana na Islamic State ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza vilipuzi, au mabomu, ambayo kundi hilo limetumia kufanya mashambulizi mabaya siku za nyuma, jeshi lilisema Jumapili.
Mpiganaji huyo, Anywari Al Iraq, raia wa Uganda, alikamatwa katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako kundi la waasi la Allied Democratic Forces lina makao yake, jeshi la Uganda People's Defense Forces, lilisema katika taarifa yake.
"Aina mbali mbali ya vifaa vya kutengenezea vilipuzi vilivyoboreshwa (IED) vilipatikana," taarifa hiyo ilisema.
Wakati wa operesheni hiyo, watu tisa wakiwemo watoto pia waliokolewa kutoka eneo la jimbo la Ituri mashariki mwa Kongo, jeshi lilisema.
Waasi wa ADF walianza kama uasi nchini Uganda lakini wamejikita nchini Congo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990.
Kundi hilo linaaminiwa kudai utiifu kwa wanamgambo wa Daesh katikati ya 2019 na inashutumiwa kuwaua mamia ya wanakijiji katika uvamizi wa mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni.
Mnamo 2021, jeshi la Uganda lilianzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi mashariki mwa Congo kujaribu kuwadhibiti waasi.