Uganda imetangaza mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola katika mji mkuu wa Kampala.
Ebola, ambao huenezwa kwa njia ya kugusa majimaji ya mwili kama vile damu, matapishi, jasho,mate,machozi, mkojo au kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo, hujidhihirisha kupitia dalili mbalimbali zikiwemo homa kali, kulegea mwili, maumivu ya misuli na kuumwa kichwa na kutoka na vidonda kooni.
" Aliyethibitika kuambukizwa na ni muuguzi wa kiume mwenye umri wa miaka 32, ambaye pia ni mfanyakazi katika hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Mulago," alisema Diana Atwine, Katibu Mkuu Wizara ya Afya nchini Uganda.
Imeripotiwa kuwa mgonjwa huyo alienda katika hospitali tatu na pia kwa mganga wa kienyeji kwa nia ya kutafuta tiba.
" Mgonjwa huyo alionesha dalili za maumivu ya kifua huku akipumua kwa shida hali iliyopelekea kutoka kwa damu nyingi sehemu mbalimbali za mwili wake," alisema Atwime wakati akizungumza na vyombo vya habari.
Hata hivyo, mgonjwa huyo alifariki Januari 29, 2025 wakati akipokea matibabu katika hospitali ya Mulago.
" Sampuli zilizotolewa kwenye mwili wake zimethibitisha kuwa alikuwa na virusi vya Ebola Sudan. Kwa sasa, hakuna mhudumu wa afya au mgonjwa mwingine yeyote kwenye wodi hiyo aliyeonesha dalili kama hizo," Atwine aliongezea.
Takriban watu 44 waliowasiliana na mwathiriwa wametambuliwa, wakiwemo wafanyakazi 30 wa afya na wagonjwa katika Hospitali ya Mulago, kulingana na Wizara ya Afya ya Uganda.
Wizara ya afya imesema imeunda timu ya usimamizi jijini Kampala huku ingine ikipelekwa maeneo ya Wakiso na Mbale ambapo mgonjwa huyo alienda kwa hospitali tofauti
" Marehemu atazikwa salama na kwa heshima ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na Utoaji wa chanjo kwa wote waliowasiliana na marehemu dhidi ya Ebola utaanza mara moja," Atwine aliongeza.
Januari 11, 2023 Uganda ilitangaza kudhibiti mlipuko wa Ebola baada ya siku 114 za kusambaa kwa maambukizi hayo.
Nchi hiyo imeshuhudia milipuko kadhaa ya ugonjwa huo, ikiwemo mwaka 2000 ambapo mamia walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa Ebola uligunduliwa mwaka 1976 katika milipuko miwili ya wakati mmoja huko Sudan Kusini na Congo, ambapo ilitokea katika kijiji karibu na Mto Ebola, ambao ndio chimbuko la jina la maradhi hayo.