Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja ameliambia bunge la nchi hiyo kuwa wilaya 82 hazina huduma ya hospitali kuu ya umma.
Amesema serikali inahitaji zaidi ya Sh6.743Trn (zaidi ya $1.8 bilioni ) kwa ajili ya kujenga hospitali kuu katika wilaya hizo.
“Makadirio ya gharama za ujenzi na vifaa vya hospitali kuu ya taifa ni Shs70Bn," Nabbanja alisema.
"Ili kufanya kazi kikamilifu katika hospitali kuu, tunahitaji fedha kwa ajili ya mishahara, matumizi yasiyo ya mishahara, dawa na vifaa vya afya vinavyokadiriwa kufikia UGX12.238Bn ( zaidi ya $3.2 milioni)," aliongeza.
Mpango wa serikali sasa ni kuboresha vituo vya afya na kuwa hospitali kuu kwa awamu, kuanzia wilaya zenye idadi kubwa ya watu.
Nabbanja alitoa ufafanuzi huo wakati katika kikao cha bunge, alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na mbunge wa Kaunti ya Omoro, akitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuboresha kituo cha afya hadi kiwango cha hospitali za wilaya kwa maeneo ambayo hazipo.
Nabbanja alibainisha kuwa kuna hospitali kuu za umma 47, hospitali za rufaa za mikoa 16, hospitali za rufaa za taifa 5 na hospitali maalumu 4 za taifa.
Amesema kwamba mwongozo na maagizo ya mkakati wa Rais yaliyotolewa mwaka 2016 yanaitaka kila wilaya kuwa na hospitali kuu.