Serikali ya Uganda imehusisha hali duni ya baadhi ya hospitali nchini humo, kutokana na Benki ya Dunia kufuta ufadhili wa Dola za Marekani milioni 90 (Shilingi bilioni 328.567) mwaka 2013.
Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja ameliambia Bunge la Taifa kuwa fedha hizo zililenga ukarabati wa hospitali chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Afya ya Uganda (UHSSP), ambayo ilitakiwa kutekelezwa kuanzia Agosti 2010 hadi Juni 2017.
"Ukarabati wa kina na vifaa vya hospitali kuu ulijumuishwa katika Mpango Mkakati wa Wizara ya Afya 2020/21 - 2024/25 kama moja ya miradi mikuu. Hata hivyo, kwa sababu ya rasilimali chache, hatujaweza kukarabati hospitali nyingi zilizopangwa ikiwa ni pamoja na ile katika wilaya ya Pallisa," Nabbanja alielezea.
"Hii imeingizwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya nne (2025/26 hadi 2029/30) kwa ajili ya kuzingatia fedha,” alifafanua zaidi.
“Wizara iliwasilisha ombi la nyongeza ya fedha kiasi cha Dola za Marekani milioni 90 (UGX328.567Bn) kwa Wizara ya Fedha, ambayo ilifaa kuwasilisha kwa Benki ya Dunia kwa ajili ya Zabuni za Awamu ya Pili ya kazi za kiraia ambayo zilitarajiwa kutangazwa hadi mwisho wa 2013," Nabbanja amesema.
"Hata hivyo, ufadhili huu wa ziada ulizuiwa na Benki ya Dunia. Juhudi zote za kutaka ufadhili huu wa ziada kurejeshwa na Benki ya Dunia hazikuzaa matunda,” alifafanua Nabbanja.
Agosti 2023, Benki ya Dunia ilitangaza kusitisha ufadhili wowote nchini Uganda, kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Kupambana na Mapenzi ya Jinsia Moja 2023,
Ilidai kuwa sheria hiyo yenye utata haiambatani kimsingi na maadili ya Kundi la Benki ya Dunia, na Maono ya kuondoa umaskini.