Wizara ya Fedha ya Uganda imesema kuwa uamuzi wa kuwasamehe wabunge kulipa ushuru wa mishahara yao umeifanya Uganda kupoteza zaidi ya Shs638.6Bn ( zaidi ya $ 171 milioni) ya kodi katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.
Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2016, yalipitisha kuwa wabunge walikubali kusamehewa mishahara yao kutokatwa kodi, kwa madai kuwa hatua hiyo ingewaondolea wabunge mzigo wa kulipa kodi na kupunguza gharama katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ripoti ya wizara hiyo pia ilionyesha kwamba wananchi wamepoteza mapato ya zaidi ya bilioni shilingi 965.65 za Uganda ( zaidi ya $259 milioni) kufuatia msamaha wa kodi uliotolewa kwa maafisa katika mashirika ya usalama, huku bilioni shilingi 30.340 za Uganda ( zaidi ya $8.1 milioni) zikitolewa katika msamaha wa kodi kwa maafisa wa Mahakama.
Kulingana na sheria hiyo mbali na wabunge, maafisa wa mahakama, wanajeshi , polisi wa magereza, na pia maafisa wa mashirika mengine ya usalama hawalipi ushuru.
"Thamani ya mapato yaliyokosekana kutokana na matumizi ya kodi inakadiriwa kufikia trilioni shilingi 2.972 za Uganda,( $797 milioni) sawa na asilimia 1.62% ya Pato la Taifa," ripoti hiyo iliongezea.
"Jumla ya kodi iliyokusanywa mwaka wa 2022/23 ni triioni shilingi 23.733 za Uganda (zaidi ya $6.3 bilioni) kumaanisha kuwa thamani ya mapato imetolewa kutokana na matumizi ya kodi ni sawa na karibu 12.5% ya jumla ya makusanyo ya kodi kulingana na makadirio," ripoti imesema.