Tume ya Haki za Kibinadamu ya Uganda (UHRC) imeliomba Bunge kupiga marufuku biashara yoyote ya uzazi wa kulipwa nchini Uganda, ili kuwalinda wasichana na wanawake dhidi ya unyanyasaji na biashara haramu dhidi ya binadamu.
Mpango huo utahusisha mwanamke mwenye siha njema kubeba ujauzito kwa niaba ya wanandoa na baada ya kurejesha mtoto au watoto kwa wanandoa hao.
" Unajua Waganda, sisi ni wepesi wa kuona kila kitu kama fursa ya biashara. Kwa hivyo tunatarajia kwamba tutaona makampuni, yakiajiri wasichana kwa shughuli za uzazi," anaeleza Ruth Ssekindi, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Ukaguzi wa UHRC.
Kulingana na UHCR, mzazi mtarajiwa, atakuwa na haki ya kuamua kulipwa au kutolipwa baada ya kubeba ujauzito.
" Biashara ya uzazi wa malipo kimataifa ni jambo kubwa sana kwa sasa. Kwa bahati mbaya, hii imesababisha unyanyasaji na usafirishaji haramu wa wanawake, na Tume inapendekeza kwamba muswada unapaswa kupiga marufuku biashara yoyote ya uzazi wa malipo au uanzishwaji wa kampuni zinazosambaza akina mama wajawazito," Ssekindi aliimbia kamati ya bunge ya nchi hiyo.
Mfumo wa kisheria wa Uganda haudhibiti kwa uwazi uzazi wa malipo, yaani si haramu wala hairuhusiwi waziwazi. Walakini, inafanywa kwa njia isiyo rasmi.
Tume hiyo pia ilipendekeza kwamba akina mama wajawazito wawe wamejifungua angalau mtoto mmoja kama kigezo kabla ya kukubali kubeba ujauzito kwa malipo.
Hatua hii inalenga kuwalinda akina mama wajawazito dhidi ya hatari za kutopata watoto wao wenyewe kutokana na matatizo yanayoweza kutokea ambayo yanaweza kuwasababishia matatizo wakati wa kubeba mimba za malipo.