Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, akipokea matibabu katika hospitali ya Mt Francis, mjini Kampala, Septemba 3, 2024./Picha: Reuters     

Tume ya Haki za Binadamu nchini (UHRC) imeunda timu maalumu ya kuchunguza shambulio dhidi ya Rais wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo, Mariam Wangadya nia ni kufahamu dhamira ya shambulizi hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki katika eneo la Kira, jijini Kampala nchini Uganda.

“Kwa sasa hatuna taarifa za kina kuhusu tukio hilo. Tunasikia vitu tofauti kutoka upande wa Jeshi la Polisi na chama cha NUP. Nilichongundua kuwa hili halikuwa tukio la kawaida na ndio maana tunaunda timu maalumu ya uchunguzi itakayoandaa ripoti maalumu.”

Mwenyekiti huyo wa UHRC amesisitiza kuwa Bobi Wine ni kiongozi wa taifa na sio tu Rais wa NUP na kwamba chochote kitakachomtokea kina maslahi kwa Waganda wote.

Wangadya amesema kuwa timu hiyo itafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na kuchukua hatua stahiki baada ya ripoti kutoka.

Bobi Wine alijeruhiwa siku ya Septemba 3 katika eneo la Manispaa ya Kira jijini Kampala nchini Uganda, alipokuwa ameenda kumtembelea mwanasheria wa chama cha NUP, George Musisi.

Kulingana na Musisi, polisi walirusha mabomu ya machozi kwa wafuasi wa chama cha NUP baada ya Bobi Wine kutoka nje ya gari yake ambapo alijeruhiwa.

TRT Afrika