Rais Yoweri Museveni ameomba kitengo cha sheria nchini humo kuisaidia serikali kupambana na ufisadi kwa kutoa adhabu kali kwa wale wanaoshitakiwa na ufisadi,
" Inspekta mkuu wa serikali anakadiria kuwa nchi inapoteza zaidi ya dola trilioni 1.8 (Shilingi trilioni 9.7) kwa mwaka kwa sababu ya ufisadi. Hili halikubaliki," Rais Museveni amesema katika mkutano wa pamoja wa kujadili uongozi, ambao unafanyika katika Taasisi ya Taifa ya Uongozi, Kyankwanzi.
" Tunahimiza kitengo cha sheria kutuunga mkono kupiga vita ufisadi, haswa katika suala la wizi wa pesa za uma, na kulifanya liwe kosa ambalo mhalifu hawachiliwi kwa dhamana ," Rais Museveni aliambia mawaziri.
Rais amesema ufisadi ambayo Uganda inakabiliana nayo ni ya aina mbili.
"Aina ya kwanza ni wizi wa fedha za Serikali, kupokea rushwa kutoka kwa Umma ili kutoa huduma za serikali, kutumia vibaya taratibu za manunuzi kudanganya serikali na kuuza kazi za serikali na kutoa kazi za serikali kwa kupendelea." Rais museveni ameelezea.
Rais Museveni amesema ufisadi aina nyengine ni wa rushwa.
" Hii ni kutokuwa mwaminifu kwa wafanyakazi katika kampuni binafsi. Wafanyakazi wanaoibia waajiri wao, pia ni maadui wa nchi. Iwapo waajiri wameorodhesha Uganda kuwa nchi ambayo wafanyikazi huiba pesa kutoka kwa waajiri wao bila kuadhibiwa, uchumi wa Uganda utadumaa," Museveni ameambia mawaziri wake.
"Kwa hiyo, ni kazi ya Polisi kuhakikisha wanaoiba makampuni ya watu binafsi au ya serikali, wanawajibishwa kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kulipa fedha walizoiba, pamoja ba na kufungwa gerezani."
Rais amesema mbali na kitengo cha kupambana na Rushwa cha Ikulu, pia anaunda kitengo cha uchunguzi wa kodi na kitengo cha uhasibu na ukaguzi.
Jukumu lake amesema litakuwa kuchunguza ukwepaji wote wa kodi, na fedha zilizoelekezwa na Bunge na baadaye kuibiwa.