Uganda ni nchi ya Afrika Mashariki ambayo ina idadi ya watu zaidi ya milioni 49. Tangu ipate uhuru mwaka 1962 imekuwa na marais 9.
Rais wa sasa Yoweri Museveni alichukuwa hatamu ya uongozi mwaka 1986.
Rais Museveni anaongoza nchi ambayo pia inatambua uongozi wa kimila wa Ufalme wa Buganda ambao unatambulika kama moja ya falme kubwa nchini humo na Afrika Mashariki.
Ufalme wa Buganda ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka 3000 hata kabla ya enzi ya ukoloni, Kabla ya uhuru ulikuwa unajiongoza lakini kufuatia uhuru wa Uganda mnamo 1962, ufalme huo ulifutwa na Waziri Mkuu wa kwanza wa Uganda Milton Obote mnamo 1966.
Rais Museveni alipoingia madarakani 1986, aliwarejeshea watu wa kabila la Baganda fahari yao kwa kurejesha ufalme wao mwaka wa 1993.
Masuala muhimu kuhusu ufalme huu
Ufalme wa Buganda ni ngome ya utamaduni wa zaidi wa watu milioni 14 wa kabila la Baganda nchini humo. Mfalme anaitwa Kabaka. Tangu kurejeshwa kwa ufalme huo, mfalme wa Buganda amekuwa Kabaka Muwenda Mutebi wa pili.
Yeye ni mfalme wa 36 wa Ufalme huo. Mke wake malkia wa sasa, anaitwa Sylvia Nagginda.Ufalme wa Buganda ni mkubwa, unasambaa katika zaidi ya wilaya 25 nchini Uganda. Kindani Buganda imejigawa ufalme wake chini ya kaunti 18.
Utawala wa Kabaka hutimizwa na waziri mkuu, bunge la ufalme linalofanya kazi na baraza la mawaziri.
Kabaka pia anaongoza kupitia wakuu wa koo kuhakikisha kwamba mila na desturi zote za watu wa Baganda zinazingatiwa na kufuatwa. Kuna wakuu 56 wa koo 56.
Ukifika jijini Kampala hakikisha umekula matooke, yaani ndizi, ambayo hupikwa kwa njia tofauti. Hicho ndiyo chakula maalum cha Baganda, Mfalme ana kasri yake kuu katika eneo la Mengo, Kampala.
Lakini pia ana kasri nyengine katika maeneo mengine ya ufalme wake. Mfalme hutokea hadharani iwapo tu ataamua kufanya hivyo.
Sherehe ambazo watu wa Buganda hungoja kwa hamu ni pamoja na sherehe yake ya kuzaliwa kila mwaka ambapo yeye hujitokeza kushiriki na wafuasi wake.
Takriban dakika thelathini kwa gari kutoka Jiji la Kampala, kuna eneo linaloitwa Nagalabi.
Hapa ndipo wafalme wote wa Buganda hutawazwa. Watu wa Buganda wanaamini ufalme wao ulianzia hapo kati ya karne ya 14 na 15.
Watu wa ufalme huu wanaamini kuwa Mfalme huzaliwa sio kuteuliwa. Kulingana na taratibu za ukoo, tayari wanajua yule ambaye atakuwa mfalme, baada ya mfalme Muwenda mutebi wa pili wa sasa.
Mtoto wake wa kiume Richard Ssemakokiro atachukua hatamu wakati ukitimia. Alizaliwa mwaka 2011.
Mfalme huwa hahudhurii mazishi. Kuna barabara moja inayoitwa Nabulagala mjini Kampala ambapo mfalme wa Buganda haruhusiwi na tamaduni yake kupita, kwa sababu inaashiria barabara ya majonzi, ambayo anaweza kupitishwa tu akiwa amekufa.
Mfalme huzikwa katika makaburi ya kifalme ya Kasubi. Eneo hili lina takriban hekta 30 ya ardhi katika eneo ambalo mwaka 1882 ilikuwa jumba la wafalme, lakini ikabadilishwa miaka miwili baadae na kuwa eneo la kupumzishwa kwa familia za kifalme. Mbali na falme hiyo,
Uganda pia ina falme nyengine ndogo ndogo ikiwemo Toro, Acholi, Bunyoro Kitoro ambazo zote zinatambulika na serikali.