Uganda imetia saini mkataba na chama cha wafanyabiashara kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kujenga uwanja mpya wa ndege wa kimataifa, ofisi ya Rais Yoweri Museveni ilisema Ijumaa.
Makubaliano ya uwanja wa ndege wa tatu wa aina hiyo katika taifa hilo la Afrika Mashariki yanapanua wigo wa kiuchumi wa UAE zaidi ya maslahi yake katika tasnia ya nishati mbadala na mafuta na gesi.
'' Hii MoU hii ni ishara ya kuimarika kwa mahusiano na washirika wetu wa Ghuba na fursa nyingine ya kushirikiana katika uwekezaji na biashara,'' alisema rais Yoweri Museveni katika taarifa katika mtandao wa X.
Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha UAE cha Sharjah kitajenga uwanja huo wa ndege nje kidogo ya Mbuga ya Kitaifa ya Kidepo kaskazini mashariki karibu na mpaka wa Uganda na Kenya, ofisi ya Museveni ilisema katika taarifa yake, bila kutoa gharama.
Uganda ina takriban viwanja 12 vya ndege kwa jumla zikiwemo viwanja vidogo vya vijiji na mbugani.
kati ya viwanja hivyo, Uwanja wa Entebbe pekee ndio mkubwa wenye uwezo wa kubeba safari za Kimataifa,
Uwanja wa Kimataifa wa Entebbe upo takriban kilomita 6 (3.7 mi) kusini-magharibi mwa mji wa Entebbe, kwenye mwambao wa kaskazini wa Ziwa Victoria.
Kwa sasa uwanja huo wa Entebbe unapokea takriban safari 27000 za kutoka kwa mashirika 19 ya ndege huku ukipokea zaidi ya abiria milioni 1.6 kwa mwaka.
Uwanja huo ulijengwa enzi za ukoloni katika mwaka wa 1951 japo kwa sasa unaendelea na mpango wa kusasisha huduma zake na ukarabati na ujenzi wa vituo vya mapokezi ya ndege na abiria kuongezea viwili vilivyoko.
Ukarabati huo unaofanywa kwa awamu kwa kandarasi na serikali za Korea Kusini na China kwa gharama ya zaidi ya dola Milioni 580, na unatarajiwa kukamilika mwaka 2030.
Uwanja wa Arua pia una uwezo wa kupokea safari za kimataifa japo kwa kiasi kidogo.
Ujenzi wa uwanja huu mpya unatazamiwa kupanua zaidi nchi hiyo kiuchumi na kuinua sekta ya mafuta, kilimo na utalii.