Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekubaliana kuwaondolea raia wa nchi mbili hizo malipo ya viza ya usafiri ili kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo.
Hatua hii ni ushindi mkubwa kwa raia wa DRC ambao, hapo awali, tofauti na raia wa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, walilazimika kulipia viza ya kwenda au kupitia Afrika Mashariki.
Makubaliano ya nchi hizo mbili yanajiri baada ya uamuzi wa hivi majuzi wa mataifa ya Kenya na Tanzania wa kuwaondolea raia wa DRC viza ili kurahisisha usafiri wa watu na kuimarisha biashara kati ya mataifa hayo.
Kenya iliwaondolea raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mahitaji ya viza kuanzia tarehe 1 Septemba, 2023.
Uganda na DRC ziliafikiana katika kikao cha nane cha Tume ya Pamoja kati ya serikali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda kilichowezeshwa kupitia mwaliko wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kufanyika mjini Kinshasa kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 12 hadi 14 Oktoba 2023.
Naibu Waziri Mkuu wa kwanza wa Uganda ambaye pia ni Waziri wa masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rebecca A. Kadaga, aliongoza ujumbe wa serikali ya Uganda katika mkutano wa nchi hizo mbili uliofanyika Kinsasha.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa DRC Antipas Mbusa Nyamwisi aliongoza ujumbe wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye mkutano huo.
Pande hizo mbili zilikubaliana kuondoa ada ya visa ya kuingia kwenye misingi ya pande zote ili kuwezesha usafiri wa watu usiokuwa na gharama.
Wakati huo huo, mataifa hayo mawili pia yalijadili ushirikiano katika nyanja za biashara, ushuru, forodha, usafirishaji, mawasiliano, tasnia, kilimo, uvuvi na mifugo, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira katika eneo la mpaka, ujenzi wa miundombinu ya umeme na barabara kati ya nchi hizo mbili. Maendeleo ya miundombinu, uchunguzi wa hidrokaboni katika maeneo ya maslahi ya kawaida na katika maswala ya kiafya pia ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa.
"Kuvuka Afrika Mashariki kunapaswa kuwa bila gharama. Unalipa viza wakati wa kwenda Amerika, au Ulaya, lakini viza kwa DR Congo? Hiyo ni takataka. Ikiwa ndivyo ilivyo, nimeiondoa," alisema rais Museveni mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa akizindua mpaka wa eneo la Mpondwe-Lhubiriha katika wilaya ya Kasese.
Mpango huu ambao umezaa matunda, mazungumzo yake yalianza kati ya marais wa nchi mbili hizo.