Kiiza Besigye amekuwa mpinzani mkuu wa kisiasa wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni / Picha: Wengine 

Msemaji wa jeshi nchini Uganda amesema mwanasiasa maarufu nchini humo Kiiza Besigye anafikishwa mbele ya Mahakama ya Jeshi Jumatano.

"Nenda kwenye mahakama ya kijeshi ya Makindye leo saa tano asubuhi, utapata jibu unalohitaji," Brigedia Felix Kulaigye alisema alipoulizwa na Mtandao wa Redio Uganda kuhusu mahali alipo Besigye.

Mashtaka yake hayajulikani.

Hii inafuatia malalamiko ya familia yake wakitaka serikali ya Uganda iseme alipo Besigye.

"Ninaomba serikali ya Uganda kumwachilia mume wangu Dr Kizza Besigye kutoka mahali anapozuiliwa mara moja. Alitekwa nyara Jumamosi iliyopita alipokuwa Nairobi kwa ajili ya uzinduzi wa vitabu vya Mheshimiwa Martha Karua," Winnie Byanyima amesema katika akaunti yake ya X.

Byanyima ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia ugonjwa wa Ukimwi, UNAIDS.

"Sasa nimearifiwa kwa uhakika kwamba yuko katika jela ya kijeshi huko Kampala. Sisi familia yake na wanasheria wake tunadai kumuona. Yeye si mwanajeshi. Kwa nini anazuiliwa katika jela ya kijeshi?" Byanyima aliuliza.

Kiiza Besigye ni nani?

Warren Kizza Besigye Kifefe alizaliwa 22 Aprili 1956, anajulikana kama Kanali Dkt. Kizza Besigye, ni daktari wa Uganda, mwanasiasa, na afisa wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda.

Kizza Besigye amekamatwa na polisi mara kadhaa kwa sababu ya shughuli zake za kisiasa/ Picha: Wengine 

Mnamo Oktoba 2000, Besigye alitangaza kwamba atashindana na Museveni katika uchaguzi wa 2001. Alistaafu kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda mwaka 2001, baada ya kufikia cheo cha kanali.

Aliwahi kuwa rais wa chama cha siasa cha Forum for Democratic Change (FDC) na alikuwa mgombea wa urais chini ya chama hicho katika chaguzi za urais za 2001, 2006, 2011 na 2016. Wakati wote alishindwa Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa Rais wa Uganda tangu 26 Januari 1986.

Besigye amekamatwa mara kadhaa

Mnamo Juni 2001, Besigye alikamatwa kwa muda mfupi na kuhojiwa na polisi kwa madai ya uhaini.

Mnamo Agosti 2001, Besigye alitoroka kutoka Uganda, akidai anahofia kuteswa na serikali. Alisema anahofia maisha yake. Aliishi Afrika Kusini kwa miaka minne, wakati huo aliendelea kuikosoa serikali ya Museveni. Besigye alirejea Uganda tarehe 26 Oktoba 2005, katika wakati muafaka kujiandikisha kama mpiga kura katika uchaguzi wa 2006.

Kampeni ya Besigye ya urais ilisimama ghafla tarehe 14 Novemba alipokamatwa kwa tuhuma za uhaini na ubakaji. Shtaka la ubakaji lilihusiana na shtaka la 1997 la binti ya rafiki aliyekufa.

Kiiza Besigye alikuwa mgombea wa urais chini ya chama cha FDC katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2001, 2006, 2011 na 2016/ Picha : AP 

Mashtaka ya uhaini yalihusu madai kuwa alikuwa na uhusiano na kikundi cha waasi cha People's Redemption Army na chengine cha Lord's Resistance Army cha Uganda.

Kukamatwa kwake kulizua ghasia mjini Kampala na kote nchini. Rais wa Uganda Yoweri Museveni alishutumiwa kwa kuibua mashtaka yasiyo na uhalisia dhidi ya Besigye katika jaribio la kumdhalilisha au kumzuia asigombee katika uchaguzi huo.

Tarehe 25 Novemba, mahakama kuu ya Uganda ilimpa Besigye dhamana, lakini alirudishwa jela mara moja kwa tuhuma za kijeshi za ugaidi na kumiliki silaha kinyume cha sheria. Besigye alikanusha mashtaka na amedai kuwa kama mstaafu kutoka kwa jeshi, hapaswi tena kufikishwa katika mahakama ya kijeshi. Aliachiliwa kwa dhamana na mahakama kuu tarehe 6 Januari.

Winnie Byanyima, mke wa Kiiza Besigye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia ugonjwa wa Ukimwi, UNAIDS/ Picha: AFP 

Besigye alikamatwa tena tarehe 28 Aprili 2011, wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.

Besigye alikamatwa tarehe 1 Oktoba 2012 baada ya kujaribu kutoa hotuba kwa wachuuzi katika soko la Kiseka mjini Kampala.

Mnamo Mei 11, 2016, Besigye alijiapisha kwa siri kuwa rais wa Uganda, siku moja kabla ya sherehe za kuapishwa rasmi kwa Rais Museveni. Alikamatwa na Jeshi la Uganda wakati wa kujiapisha.

Mnamo Mei 2022, Besigye alikamatwa wakati wa maandamano juu ya kupanda kwa bei ya bidhaa nchini Uganda.

TRT Afrika