Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alitoa utambulisho wa washukiwa hao. Picha/Polisi wa Uganda

Polisi nchini Uganda wamewazuilia maafisa tisa wa wizara ya fedha ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa tuhuma za kudukua mifumo ya kielektroniki ya benki kuu iliyosababisha wizi wa shilingi bilioni 62 (dola milioni 16.87), wizara na polisi zilisema.

Mnamo Novemba mwaka jana, Waziri wa Jimbo la Fedha Henry Musasizi alithibitisha ripoti katika vyombo vya habari vya ndani kwamba akaunti za benki kuu zilidukuliwa na pesa kuibiwa.

Waliozuiliwa ni pamoja na afisa mkuu wa idara ya Hazina ya wizara hiyo, polisi na wizara ya fedha ilisema.

Baadhi ya maafisa walio katika afisi ya mhasibu mkuu katika wizara hiyo "waliitwa na kuzuiliwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai ili kuwezesha kukamilika kwa uchunguzi," wizara ya fedha ilisema kwenye chapisho kwenye akaunti yake ya X jioni ya Jumanne.

Wizara haikutoa majina ya waliozuiliwa wala idadi yao.

Majina yalisomwa

Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke, hata hivyo, aliambia televisheni ya NTV kwamba maafisa tisa wamezuiliwa na pia kusoma majina yao ambayo ni pamoja na afisa mkuu wa Hazina.

Afisa huyo na wengine wanane waliokamatwa hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao.

Gazeti la serikali la New Vision liliripoti kwamba wadukuzi, wakijitambulisha kama "Taka", walipata mifumo ya IT ya Benki ya Uganda na kuhamisha fedha hizo kinyume cha sheria.

TRT Afrika