Kesi ya Kiiza Besigye na msaidizi wake, Hajj Obeid Lutale inayohusu makosa ya usalama na kumiliki silaha kinyume cha sheria. Picha: Reuters

Kesi ya mwanasiasa mkongwe wa Uganda Dkt. Kiiza Besigye na msaidizi wake Obeid Lutale, imeahirishwa hadi Januari 13, 2025, kwa ajili ya kutajwa zaidi.

Wawili hao wamefikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini kampala nchini Uganda.

Zaidi ya mawakili 40 wanamuwakilisha Besigye na msaidizi wake, Hajj Obeid Lutale, katika kesi yao inayohusu makosa ya usalama na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Kati yao ni wakili kutoka Kenya, Martha Karua ambaye alipata cheti cha kutoa huduma ya kumwakilisha Besigye katika kesi yake iliyosikizwa Januari 6, 2025.

Hii ni baada ya Baraza la Sheria Uganda kukataa kumpa cheti hicho Disemba 2024 ikidai kuwa hajatimiza mahitaji yote.

Hapo awali wanaomuunga mkono Dkt. Kizza Besigye waliimba katika Mahakama Kuu ya Kijeshi jijini Kampala, baada ya baadhi ya mawakili kunyimwa kuingia.

Wakili akamatwa

Mmoja wa wakili anayemtetea Besigye alikamatwa kwa madai ya kukiuka sheria. Eron Kiiza alikamatwa ndani ya mahakama hiyo ya kijeshi kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.

Awali Kiiza alizuiliwa kuingia mahakamani, baadaye akavutwa na kutupwa nje, na baadaye kuwekwa kizuizini pamoja na kina Besigye. Baada ya muda Kiiza alitolewa na kupelekwa mahali pasipojulikana.

Mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu wakili huyo.

TRT Afrika