Uganda Ebola vaccine trial photo by Tedros Adhanom

Wizara ya Afya ya Uganda, Shirika la Afya Duniani (WHO) na washirika wengine leo wanaendelea na majaribio ya kwanza kabisa ya chanjo ya Ebola kutoka kwa aina ya virusi vya Ebola Sudan.

Watafiti wakuu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere na Taasisi ya Utafiti wa Virusi vya Uganda (UVRI), kwa usaidizi kutoka WHO na washirika wengine, wamekuwa mbioni kufanya majaribio tayari ndani ya siku 4 tangu kuthibitishwa kwa ugonjwa huo mnamo Januari 30.

" Ni jaribio la kwanza kutathmini ufanisi wa kiafya wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola kutokana na virusi vya Sudan. Kasi hiyo ilifikiwa kupitia utayari wa hali ya juu wa utafiti, huku ikihakikisha ufuatiliaji kamili wa mahitaji ya kitaifa na kimataifa ya udhibiti kwa kuzingatia utaratibu," WHO imesema katika taarifa.

Watu watatu hadi sasa wameripotiwa kuambukizwa Ebola nchini Uganda, huku mgonjwa wa kwanza akifariki.

Aina tofauti ya Ebola

Chanjo zilizoidhinishwa zinapatikana tu kwa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Ebola, ambavyo zamani vilijulikana kama Zaire ebolavirus.

Vile vile kwa matibabu yaliyoidhinishwa yanapatikana kwa virusi vya Ebola pekee.

Kuna chanjo mbili zilizoruhusiwa kutumika kwa wagonjwa wenye Ebola aina ya Zaire.

" Kwa vile milipuko ya Ebola ni ya nadra na haitabiriki, na kutokana na idadi ndogo ya chanjo, chanjo ya Ervebo ya Ebola Zaire imetengwa kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko ili kuwalinda watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa Ebola chini ya mkakati ambao ni sawa na mbinu inayotumika kutokomeza ugonjwa wa ndui, " WHO imesema.

Lakini hakuna chanjo iliyoidhinishwa kwa Ebola aina ya Sudan na ndiyo sababu majaribio ya chanjo yanafanyika.

"Hii inaashiria hatua kubwa katika kukabiliana na masuala dharura ya afya na inaonyesha nguvu ya ushirikiano kwa usalama wa afya duniani," Dkt. Matshidiso Moeti alisema. "Ikithibitishwa kuwa na ufanisi, chanjo hiyo itaimarisha zaidi hatua za kulinda jamii kutokana na milipuko ya siku zijazo."

Dozi 2,160 za kwanza za chanjo zitatumiaka katika majaribio na WHO tayari imetenga dola za Marekani milioni 1 kutoka Mfuko wake wa Dharura kwa ajili ya kusaidia kuharakisha juhudi za kudhibiti milipuko.

TRT Afrika