Chama tawala nchini Uganda kimeazimia kulinda kura za Rais Yoweri Museveni wakati wa uchaguzi ujao utakaofanyika mwaka 2026./Picha: Wengine

Chama tawala nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM) kinatarajiwa kuajiri zaidi ya waganda 145,000 ili kulinda kura za Rais Yoweri Museveni katika Uchaguzi Mkuu wa 2026.

Uamuzi huo unafuatia malalamiko ya Rais Museveni dhidi ya chama cha National Unity Platform (NUP) kuhusu wizi wa kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Museveni alisisitiza kuwa ana ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma dhidi ya NUP.

Wafuasi wa chama cha NRM wakiwa katika uzinduzi wa kampeni ya kulinda kura za Rais Yoweri Museveni./Picha: Wengine

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kulinda kura za Rais Museveni, mshauri mwandamizi wa Rais wa nchi hiyo, Hadija Namyalo amesema kuwa NRM inalenga kuajiri watu wa kuanzia umri wa miaka 20 hadi 40.

“Tumekumbwa na changamoto wa kubadilishiwa kura zetu na ndio maana tumeanzisha kampeni hii, mahsusi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa kwanza wa NRM Moses Kigongo, amewataka waratibu wa kampeni hiyo kuepuka vitendo vya rushwa.

“Tunafahamu kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa na tabia ya kuhonga mawakala wetu, tumejipanga kuhakikisha kuwa hilo halitokei katika uchaguzi ujao,” alisema Kigongo.

TRT Afrika