Naibu Spika wa bunge ya taifa ya Uganda Thomas Tayebwa ameongoza kikao cha bunge Jumanne ambalo limejadili kuuawa kwa mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei nchini Kenya , 5 Septemba 2024.
Cheptegei mwenye miaka 33, ambaye alishiriki Olimpiki ya Paris 2024, alifariki nchini Kenya baada ya kushambuliwa na kuchomwa na aliyekuwa mpenzi wake, Dickson Ndiema.
Naibu Spika amesema shambulio hilo linaangazia kuwa suluhu muhimu inahitajika kukomesha unyanyasaji wa nyumbani nchini Uganda.
"Inasikitisha kwamba tunaendelea kupoteza watu kwa namna hii, hasa kupitia unyanyasaji wa nyumbani. Kwa kweli, ni jambo ambalo tunapaswa kuketi na kuona jinsi tunavyoweza kushughulikia. Inasikitisha sana,” alisema Tayebwa.
"Kuna wengi wanaokufa kwa njia hiyo ambao hawajulikani. Dada yetu Rebecca angalau alikuwa na jina ambalo lingeweza kusikika zaidi ya eneo la nyumbani kwake, lakini kwa wale wanaokufa kimya kimya, ni suala ambalo tunapaswa kulishughulikia sio tu viongozi wa kisiasa bali viongozi kutoka nyanja zote za jamii, Tayebwa aliongezea.
Wanaharakati wanawake, chini ya mradi wa 'Womenprobono' walionyesha kukerwa na mauaji ya kikatili ya Rebecca na kwamba mauaji yake yameharibu mustakabali wa binti zake wawili wachanga.
"Uganda na sehemu nyingi za dunia zimeshuhudia janga la ukatili dhidi ya wanawake. Ulimwenguni, kila baada ya dakika 11, mwanamke au msichana anauawa na mpenzi wake au mtu wa familia, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu," ilisema sehemu ya taarifa ya shirika hilo la Septemba 7, 2024 .
Kulingana na Ripoti ya Polisi Uganda ya Mwaka 2023, kesi 14,681 za unyanyasaji wa kijinsia ziliripotiwa kwa Polisi wa Uganda mnamo 2023, ishara kwamba kesi 40 zilikuwa zikiripotiwa Polisi kila siku kwa wastani.
Cheptegei alizikwa akipewa heshima zote za kijeshi 14 Septemba 2024 katika wilaya ya Bukwo, Uganda.
Mji mkuu wa Ufaransa Paris, ulitoa heshima kwa mwana Olimpiki wa Uganda Rebecca Cheptegei kwa kuipa kituo cha michezo jina lake .