Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine amejeruhiwa mguuni katika makabiliano na polisi Jumanne nje kidogo katika kijiji cha Bulindo, Wilaya ya Wakiso, kundi lake la upinzani lilisema.
Picha zilizochapishwa mtandaoni zilionyesha Wine akiwa amezungukwa na wafuasi ambao walipiga kelele kwamba alipigwa risasi mguuni kabla ya baadhi yao kumuingiza ndani ya gari lililokuwa likimsubiri.
Chama chake, National Unity Platform, ndicho chama chenye viti vingi zaidi kuliko vyama vyote vya upinzani katika bunge la kitaifa. Chama hicho kilisema kwenye mtandao wa X kwamba maafisa wa usalama wa Uganda "wamefanya jaribio la kumuua" Wine, ambaye jina lake halisi ni Kyagulanyi Ssentamu.
"Alipigwa risasi mguuni na kujeruhiwa vibaya huko Bulindo, Wilaya ya Wakiso," ilisema, Wakiso ni wilaya ilio nje kidogo ya mji mkuu wa Uganda wa Kampala.
Makabiliano ya barabarani kati ya Wine na polisi mara kwa mara yageuka kuwa vurugu, lakini hii ni mara yake ya kwanza kujeruhiwa kwa namna hiyo.
Hakukuwa na taarifa ya haraka kutoka kwa polisi kuhusu tukio hilo.
Wine aligombea urais mwaka wa 2021, na kushindwa na Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi aliodai uliibiwa dhidi yake. Museveni ameshikilia madaraka tangu 1986.