Kabila la Makonde nchini Tanzania linajulikana kwa utajiri wa utamaduni, historia, na sanaa. Ingawa sanaa yake ya uchongaji yenye thamani ilionekana kupungua miaka iliyopita, baadhi ya wasanii kama vile Sebastian Daniel Mbebe wanajaribu kuihifadhi - kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya Afrika.
Mbebe alirithi sanaa hiyo kutoka kwa babake na babu yake. ''Shughuli zangu zimejikita zaidi katika sanaa ya kijamii. Nilipokua, niligundua kuwa familia yangu inafuata utamaduni huu. Ndivyo nilivyokuwa msanii wa uchongaji. Niliaanza na shughuli ndogo ndogo mpaka nilikua kama fundi,'' alieleza Mbebe alipozungumza na TRT Afrika.
Anapenda sanaa hiyo.
Anatumia sanaa hii kuwasimulia hadithi za Kiafrika, kuhifadhi utamaduni, na kuinua utalii. ''Ni sehemu ya mila na utamaduni wa kabila la Makonde,'' anasema msanii huyo.
Uchongaji ni mojawapo ya sehemu kubwa za utamaduni na historia ya Kiafrika. Sebestian Mbebe hutumia miti kuunda sanamu mbalimbali - hakuna udongo, hakuna chuma.
''Hatutumii udongo. Tunatumia miti, aina yoyote ya mti, lakini kwa kawaida, tunatumia mti wa Mpingo "African blackwood" kwa sababu ni mti imara ambao unadumu kwa muda mrefu. Lakini uchongaji wake ni rahisi,'' anasema.
Anapojitahidi kuokoa sanaa inayofifia, Mbebe anahisi kuwa kuna haja kwa Waafrika kufufua upendo wao kwa sanaa ya kienyeji.
"Kwa soko la ndani, bado tunawatia moyo Watanzania na Waafrika kwa ujumla kupenda sanaa. Lakini kwa kiasi kikubwa, tunategemea soko kutoka nje," anasema.
Kazi ngumu
Kazi hiyo inahitaji ujuzi na uvumilivu mwingi kwa sababu wasanii bado wanatumia zana ambazo haziko sana. Inachukua miezi kadhaa kuunda sanamu ya kushangaza ambayo inavutia wageni wa ndani na kimataifa.
"Kwa mfano, 'Ujamaa' ina urefu wa futi sita. Kwa hiyo, ikiwa utafanya kazi kila siku, inaweza kuchukua miezi mitatu, minne, hadi mitano, kutokana na mazingira na zana tunazotumia," Mbebe anaelezea.
Anatengeneza sanamu mbalimbali kuonyesha maisha na utamaduni wa Kiafrika. ''Mama anatembea kwenda shambani, anabeba vitu, na kuna vitu tunavyotumia, kama kisago chetu cha jadi na jembe,'' anasema.
''Inaweza kuwa mama anapika huku akimtazama mtu mwingine, anamwambia: 'Usiende huko, ninapika chakula?' Basi, mambo kama hayo. Mara nyingi, tunafanya hivyo kuonyesha utamaduni na mila ya Afrika, hasa ya kabila fulani,'' Mbebe anaelezea.
Ingawa msanii huyo wa Kitanzania ana shauku ya kuhifadhi utamaduni wa Kiafrika, pia anachukulia sanaa hiyo kama biashara ili kumhudumia familia yake, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto wake.
Janga la Uviko-19 liligusa uchumi wa dunia nzima na kusambaratisha shughuli nyingi. Kwenye sanaa ya uchongaji haikuwa tofauti. Lakini Mbebe anasema mambo sasa yamebadilika.
''Bado hatujaimarika kifedha. Soko letu pia halijatulia, hata njia ambayo wateja wetu wanakuja, kabla ya Uviko ilikuwa tofauti."
Hakuna hasara
Baada ya Uviko, hali imekuwa ngumu, lakini hatujasimama. Bado tunaendelea. Tunapata faida kwa sababu tunapata pesa kidogo, watoto wanakwenda shule, maisha yanakwenda, na tunamshukuru Mungu,"
Licha ya changamoto zilizopo, Sebastian Mbebe anaamini kuwa sanaa hiyo humletea furaha kutokana na thamani yake kiuchumi na kitamaduni.
"Nguvu zangu zinatokana na sanaa. Kwa hiyo, nikizungumzia faida, ndiyo tunapata faida, hakuna hasara katika kazi yoyote ikiwa unaendelea kuifanya kila siku,"