Na Dayo Yussuf
Mnamo 2011, Wakenya waliingia katika maombolezo kufuatia kifo cha mmoja wa mtu mashuhuri, Profesa Wangari Maathai.
Lakini hawakujua kwamba habari za kushtua zaidi zingefuata.
Katika wosia wake mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel aliacha maagizo kwamba angependa mwili wake uchomwe kwenye tanuri la umeme, akiendelea na mapambano yake ya kuhifadhi mazingira hata baada ya kufariki dunia.
Uamuzi wake ulizua mjadala kote nchini, ukiangazia imani za kitamaduni na kidini zinazohusu kifo na mazishi nchini Kenya na sehemu zingine za Afrika.
Katika jamii ambapo mazishi mara nyingi huchukuliwa kuwa jambo la heshima kwa marehemu, chaguo la Maathai lilionekana kuwa lisilo la kawaida na kwa wengine, hata lenye utata.
Askofu Mark Kariuki, wa Kanisa la Deliverance Church Kenya aliwahi kunukuliwa katika gazeti la Nation, gazeti la kila siku nchini humo akisema ingawa uchomaji wa maiti haukatazwi moja kwa moja katika Biblia, unachukiza kwa waumini.
‘’Haijalishi uliliwa na wanyama, ulipotea baharini au kuchomwa moto, kilichokuwa muhimu zaidi ni uhusiano wako na Mungu…’’ Alisema Askofu Mark.
Nchini Kenya na kwa hakika sehemu nyingi za Afrika, shughuli za mazishi sio tu mila bali ni suala la kijamii linaloheshimu mababu na kudumisha utamaduni.
Mara nyingi, makaburi huwa yanaheshimiwa kama sehemu muhimu zaidi kwa walio hai, ikiashiria uhusiano wa kimwili kati ya walio hai na wafu.
Kinyume chake, uchomaji maiti, ambao mara nyingi huchukuliwa kuwa jambo la kigeni au la ajabu, kihistoria umekataliwa na jamii nyingi za Kiafrika.
Lakini hali inabadilika sasa.
Watu wengi hasa kutoka kwa vizazi vya zamani wanaona uchomaji maiti kama mtindo unaochagizwa na mataifa ya Magharibi, mtindo wa kigeni zaidi ambao wanaogopa hata kulitafakari hilo.
Vipi kuhusu Mungu? Wangeuliza. Vipi kuhusu mababu zetu na mila zetu?
Waafrika wengi bado wana mtazamo wa heshima kubwa katika suala la maisha na kifo na katika hali zingine kuwa takatifu.
Kwa mfano dini ya Kikristo, ambayo ina wafuasi wengi Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ingawa imekuwepo kwa miaka mingi na inaendelea kubadilika ili kushughulikia ukuaji wa kisasa, suala la mazishi bado linabaki kuwa la kihafidhina.
Lakini kwa dini ya Kiislamu hakuna shaka kwa hili. Uchomaji maiti hauruhusiwi kamwe.
Ustadh Shaaban Omar, Imamu mjini Nairobi, anasema Uislamu unalinda utu wa mtu hasa katika kifo.
‘’Mtu anapokufa, hakuna anachoweza kujifanyia mwenyewe. Dini yetu inatufundisha kuwa ni wajibu wetu kama jamii inayomzunguka kuhakikisha hapati aibu, hadhalilishwi au kunyanyaswa kwa namna yoyote ile,'' Ustadh Shaaban aliiambia TRT Afrika. Ni lazima tumpe mazishi ya heshima na tuyafanye haraka na rahisi iwezekanavyo,’’ anaongeza.
‘’Uchomaji maiti hauruhusiwi kwa vyovyote vile. Kwa sababu tunaamini mtu akifa, bado anaweza kusikia na kuhisi anapoguswa hata kidogo, fikiria kuchoma maiti ni sawa na kumchoma mtu akiwa hai.’’
Lakini, hoja za Profesa Maathai zilitoa mtazamo chanya. Alikuwa mwanamazingira katika uhai wake, aliona uchomaji maiti kama jambo la kutekeleza alichokiamini na la kiikolojia, linalolingana na utetezi wake wa maisha endelevu.
"Kwa nini nichukue sehemu ya ardhi wakati wa kifo wakati nimetumia maisha yangu kuilinda?" aliripotiwa kuuliza.
Uamuzi wake uliwalazimisha Wakenya wengi kukabiliana na hali halisi ya ukuaji wa miji, uhaba wa ardhi, na kubadilisha mtindo wa maisha ambao unazidi kupinga desturi za jadi za kuzika.
Katika maeneo ya mijini kama Nairobi, maeneo ya kuzika yamekuwa jambo la kero sana.
Makaburi yamejaa kupita kiasi, na ardhi kwa ajili ya makaburi mapya ni ndogo na yenye gharama kubwa.
Kupanda kwa gharama za mazishi—kuhusisha majeneza, usafiri, na masuala ya matambiko —huwa ni mzigo mkubwa wa kifedha kwa familia, na kusababisha baadhi ya watu kufikiria upya njia mbadala kama vile kuchoma maiti.
Lakini ni msukumo na mvutano kati ya kizazi cha zamani zaidi cha kihafidhina, na vijana wa sasa ambao wanajali zaidi mazingira na wanaonekana kutozingatia imani na mienendo ya kidini.
Pia katika matukio mengi, wanahisi huu ni uamuzi wa mtu binafsi ambao unatakiwa kuheshimiwa.
Na kunao sasa baadhi ya Wakristo ambao wanaacha maagizo kwamba wangependa kuchomwa moto badala ya kuzikwa.
’Katika Uislamu hatujali hayo, hata mtu akiacha wosia akisema anataka kuchomwa,’’ anasema Ustadh Shaaban. ‘’Jamii haitatekeleza maagizo fulani kwa sababu hayaambatani na dini yetu na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW),’’ anaongeza.
Nchini Kenya, kuna sehemu chache tu za kuchomea maiti, huku mojawapo ya eneo mashuhuri zaidi ikiwa katika Makaburi ya Lang’ata jijini Nairobi.
Licha ya kuwepo sehemu hiyo, aghalabu haina shughuli nyingi, huku wateja wengi wakiwa ni wahamiaji kutoka nchi za nje, Jamii ya Wahindu au watu binafsi wenye mtazamo kama wa Maathai.
Mahali pengine barani Afrika, mambo hayo yanakuwa ni nadra. Nchini Afrika Kusini, uchomaji maiti ni jambo la kawaida zaidi, haswa miongoni mwa jamii zinazoishi mijini, tabaka la kati na zisizo za Kiafrika.
Nchini Ghana na Nigeria, imani thabiti za Kikristo na za kitamaduni zinaendeleza desturi ya kufanya mazishi. Hii ni licha ya kuwepo kwa mijadala kuhusu uchomaji maiti kama jambo ambalo linasemekana kuwa litapunguza gharama na kulinda mazingira.
Mabadiliko ya taratibu kuelekea uchomaji maiti barani Afrika yanaonyesha vuta nikuvute kati ya usasa na mila.