Sur les 24 candidatures enregistrées, une seule est une femme, Marie-Josée Ifoku Mputa, déjà candidate à la présidentielle de décembre 2018. Photo : TRT Afrika

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Marie Josée Mputa Mpunga IFOKU, mwenye umri wa miaka 58 ni mgombea mwanamke katika uchaguzi wa urais wa Disemba, 20, 2023.

Baada ya kuwania urais kwa mara ya kwanza mwaka 2018, Bi Ifoku anaamini kwamba mara hii ujumbe wake utawashawishi wapiga kura, ''Mwaka 2018 sikujiandaa vizuri. Lakini uzuri nilipata jukwaa na fursa ya kuonekana. Nimezingatia mengi na kupata uzoefu. Ndio maana sikuvunjika moyo. Mara hii nimejizatiti na ninaamini nitafanya vizuri zaidi,'' anasema.

Maisha ya Ugenini

Bi Marie-Josée IFOKU alizaliwa mjini Kinshasa tarehe 6 Februari mwaka 1956.

Sehemu kubwa ya utoto wake aliishi Uholanzi na Ubelgiji kabla ya kumalizia shule yake ya sekondari mjini Kinshasa. Wazazi wake wana asili ya mkoa wa Tshuapa katika jimbo la zamani la Équateur, katikati mwa Congo. Na baba yake alikuwa mwanadiplomasia wa Congo.

Bi IFOKU baadae alikwenda Ufaransa kuendeleza elimu ya Chuo Kikuu kisha baadae Chuo Kikuu cha Quebec nchini Canada. Kote huko alijifunza taaluma za utawala.

Baada ya masomo, alifanya kazi nchini Canada katika kiwanda cha magari cha Ford.

Mwaka wa 2004, Marie-Josee IFOKU alirudi kuishi nchin mwake DRC na kuongoza kampuni ya kuuza magari ya Congo Motors.

Marie-Josee IFOKU ni mama wa familia mwenye watoto na wajukuu watatu.

Marie Ifoku mgombea urais DRC. 

Safari ya kisiasa

Mwaka wa 2015, Marie Josée IFOKU alijiunga na harakati za kisiasa na kushikilia nyadhifa za utawala katika mkoa wa Tshuapa hadi kuwa Gavana wa mkoa huo.

Baadae Bi IFOKU aliunda chama cha kisiasa cha mrengo wa kati cha Alliance des Élites pour un Nouveau Congo AENC ( Muungano wa Viongozi na Wasomi kuhusu Congo Mpya).

"Baada ya kufanya kazi katika sekta binafsi muda mrefu pamoja na kusimamia harakati katika mashirika ya kinamama niliona sehemu nzuri ya kufikia mageuzi na kufanya maamuzi ni kuunda chama na kuchangamkia siasa,'' anasema.

Kampeni ya ''Ufagio''

Bi IFOKU amejipatia umaarufu mkubwa kwenye kampeni hii ya uchaguzi kutokana na kutembea na ufagio wenye rangi za DRC kwenye kampeni zake. Lakini ufagio huo unaoitwa kwa lugha ya Lingala ''Kombo'' una maana gani?

''Ufagio au ''Kombo'' kwanza ni ishara ya utawala. Lakini pia namaanisha wakati umewadia wa '' kufagia, kusafisha na kufyeka kabisa tabia sugu ya mfumo wa uporaji uliotia mizizi nchini DRC. Ni wakati wa kuachana na maadili haramu na kuijenga Congo Mpya yenye Maadili na Utawala bora,'' anasema Marie.

Marie Ifoku amechagua fagio kama nembo yake ya kuleta mabadiliko nchini DRC. 

Kampeni yake ya '' Ufagio'' imewashawishi baadhi ya wapiga kura kama mzee Raymond Betua kutoka mkoa wa Tshuapa.

''Tangu mwaka wa 1960, wanaume walitawala nchi hii, lakini hakuna aliyeleta mabadiliko au maendeleo. Nadhani wakati umewadia wa kuwapa fursa kinamama nao kwenye uongozi wa nchi. Pengine wao wataweza pale ambapo Kinababa walifeli,'' anasema Raymond.

Na swali hilo kama kinamama kweli wanaweza ndio limekuwa mjadala maeneo yote ya kampeni ya Bi Marie- Josée IFOKU.

Aliulizwa kama yuko tayari kupambana na wanaume zaidi ya 20 kwenye uchaguzi huu na kuweza kupata kura.

''Mimi sina uoga hata kidogo. Katika kazi zangu zote nilikuwa mmoja katika kundi la Wanaume. Ukianza kwenye mauzo ya gari lakini pia katika uongozi wa mkoa. Nilikuwa pekee yangu nikizungukwa na wanaume. Lakini niliweza kusimama na kufaulu. Mimi ni shupavu na mbambanaji,'' alisema kwa kujiamini Bi IFOKU.

''Kura za wanawake sina shaka nadhani niko mtu sahihi wa kuwatetea. Na hata kwa wengine nafikiri hii ni fursa nzuri ya kuchagua mwanamke. Tuna shida nyingi zikiwemo za kijamii na mtu sahihi wa kutafuta ufumbuzi bila shaka ni mimi,'' amesema.

Ajenda ya kisiasa

Bi Marie -Josée IFOKU anasema kabla ya kupangilia ilani yake alijiuliza sana '' Kwa nini nchi yenye utajiri wa kupindukia kama Congo, lakini wananchi wake wanaishi katika umasikini mkubwa?'' Hivyo alitiririka na Ilani yake:

1.Kuelewa kwanza hali halisi ya DRC.

2.Kuwaelimisha raia changamoto mbalimbali za nchi.

3.Maridhiano ya Kitaifa.

4.Umoja katika tabaka mbalimbali nchini.

5. ''Kuisafisha''Nchi

Marie Ifoku anasema amejiuliza, "Kwa nini nchi yenye utajiri wa kupindukia kama Congo, wananchi wake wanaishi katika umasikini mkubwa?'' Picha/TRT Afrika. 

Na hapa Bi IFOKU anasema ndio mwanzo wa ''Kuijenga Congo mpya chini ya misingi ya Utawala Bora na kumuweka raia kwenye safu ya mbele.

Tofauti na wagombea wengine , Bi IFOKU anasema Mashariki mwa Congo kuna '' vita ya kiuchumi'' hivyo ''dawa nzuri '' ni ' kuwastaawisha kimaisha watu wa maeneo hayo kwa kuwajengea viwanda na kuwapa ajira na hivyo kumaliza vurugu na machafuko ya muda mrefu.

Uchaguzi huo wa Disemba 20 utashuhudia wagombea wanawake wawili katika wagombea 22. Mbali Bi Marie-Josée IFOKU, mwanamama Joëlle Bile, ambae ni mwanahabari wa zamani naye pia amejitosa kwenye kinying'anyiro hicho.

TRT Afrika