Baada ya uchaguzi wa Disemba 20 kumalizika nchini DRC, hivi sasa macho yote yanaelekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo CENI.
Kawaida, kura zimeanza kuhesabiwa punde tu baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa kumi na moja jioni, ambao kwa mujibu ya CENI ndio muda rasmi wa zoezi la kupiga kura kumaliza. Hata hivyo, kuna baadhi ya vituo ambavyo viliongezewa muda wa kupiga kura, kufuatia taarifa za kuchelewa kuanza kupiga kura kutokana na sababu mbalimbali, hivyo CENI ilitaka kufidia. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na Bunia, Mashariki mwa DRC.
"Tume ya Uchaguzi CENI inawashukuru wapiga kura waliojitokeza mapema asubuhi. Hata hivyo, imegundua kwamba kulikuwa na kuchelewa katika kuanzishwa kwa zoezi la kupiga kura katika baadhi ya vituo nchini. CENI inasema inazingatia na kubeba dhamana ya matatizo yote kuhusiana na upigaji kura," imesema CENI.
Purukushani pia zimeripotiwa kutokea katika baadhi ya maeneo Mashariki mwa DRC baada ya wakimbizi wa ndani kutaka kupiga kura katika vituo ambavyo sivyo walivyojiandikisha awali.
Kura kuhesabiwa
Kura zinaanza kuhesabiwa punde tu baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika.
Zoezi la kuhesabu kura linatakiwa kufanyika mbele ya mashahidi, waangalizi, waandishi wa habari, na mawakala, na kuhesabiwa kwa kura kunatakiwa kuendelea bila kusita mpaka pale zoezi hilo litakapokamilika, hayo ni kwa mujibu wa sheria za kura.
Baada ya hapo, matokeo yanatakiwa kutangazwa hadharani haraka iwezekanavyo katika vituo vya kupigia kura, kabla kupelekwa katika ofisi kuu ya uchaguzi ngazi ya wilaya kwa ajili ya majumuisho, na baadae makao makuu ya Tume, yaliyopo mjini Kinshasa.
Tume inachakata matokea kutoka vituo vinavyokusanya na kuandaa matokeo ya awali, ambayo lazima yathibitishwe na wajumbe wote wa bodi kabla kutangazwa rasmi hadharani.
Mkuu wa Tume anatakiwa kutangaza matokeo yote ya awali ifikapo Disemba, 31. Siku 10 baada ya uchaguzi.
Hali ikoje
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa TRT Afrika ambae yuko mjini Kinshasa, anasema mpaka sasa hali mjini humo iko shwari, ingawa shauku kubwa uliyopo kwa wananchi hivi sasa ni kuanza kusikia matokeo ya uchaguzi yakitangazwa katika vituo mbalimbali nchini humo.
Ingawa awali, baadhi ya wagombea wa urais kutoka kambi ya upinzani walionekana kuanza kulalamika na kudai kuwa zoezi la upigaji kura lilikuwa na hitilafu kadhaa, lakini waangalizi wa kutoka jumuia ya SADC wanasema kila kitu kimeenda sawa.
"Ingawa muda rasmi wa kuanza kupiga kura ni saa kumi na mbili asubuhi, lakini mpaka maafisa wanapokuwa tayari, kawaida kunakuwa na hali ya kuchelewa kuanza kupiga kura kwa takriban nusu saa. Lakini kila kitu tunaona kimeenda sawa," anasema Enoch Kavindele, mwenyekiti wa kamati kuu ya uangalizi chini ya SADC.
Matumaini ya wananchi
Licha ya shauku kubwa waliokuwa nayo wananchi ya kutaka kujua nani ataibuka kidedea katika uchaguzi mwa Disemba, 2023, lakini hamu yao pia ni kuona zoezi hili linakamilikwa kwa amani huku wakitaka mshindi kuzingatia maslahi ya nchi. Uchaguzi wa mwaka huu, umeangaliwa na wengi, ndani na nje ya bara. DRC licha ya kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kujipatia uhuru wake, mwaka 1960, lakini uchaguzi huu utakuwa ni pili kufanyika kwa amani tangu nchi hiyo kupata uhuru.
Hii ni kutokana na machafuko yaliyoikumba taifa hilo kwa miongo kadhaa. Ni kutokana na hali hiyo, ambapo suala la kurudisha amani lilionekana kupenya katika ajenda kuu ya kila mgombea.