Serekali ya DRC inataka maelezo kutoka serikali ya Kenya, baada ya tangazo la kuundwa kwa muungano wa kisiasa na kijeshi unaowajumuisha kundi la waasi wa M23 wanaoendesha harakati zao mashariki mwa Kongo. Balozi wa Kenya nchini DRC aliitwa na diplomasia ya Kongo.
Wito huu unakuja saa chache baada ya kiongozi wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Kongo, Corneille Nangaa, kuunda "muungano wa kisiasa unaojumuisha waasi wa M23."
"Serikali yetu ina haki ya kuomba maelezo kutoka kwa serikali ya Kenya kwa msaada ambao Corneille Nangaa alipokea kutoka kwa serikali yao," Christophe Lutundula, Naibu Waziri Mkuu wa Mambo ya Nje, akithibitisha kwamba balozi wa Kenya nchini DRC atatowa maelezo zaidi Kinshasa.
Akiwa uhamishoni, kiongozi wa zamani wa CENI alitangaza, Ijumaa, kuundwa kwa Muungano wa Mto Kongo, muungano wa kisiasa na kijeshi, akitoa wito wa "muungano wa vikosi vyote vya kisiasa, kijamii na kijeshi" kwa ajili ya "uundaji upya wa Jimbo" na "kurudi kwa amani."
"Nimeiagiza ofisi yangu kumpokea balozi wa Kenya nchini DRC ili kuwe na maelezo kadhaa kuhusu kile kinachoendelea, ikibidi…Hatutasita kuiarifu Kenya na kuvunja mawalisiano nao," anaongeza Naibu Waziri Mkuu wa Mambo ya Nje wa Kongo.
"Kukomesha udhaifu wa serikali"
Wakati DRC ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu tarehe 20 Disemba katika hali ya wasiwasi ya kisiasa na kiusalama, Bw. Nangaa, ambaye alikuwa kiongozi wa Tume ya Uchaguzi (CENI) wakati wa uchaguzi wa 2018, alijitokeza Ijumaa katika hoteli moja katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi akiwa na Bertrand Bisimwa, "kiongozi" wa waasi wa M23.
Muungano huu, kulingana na Bw. Nangaa, ni muhimu kukomesha "udhaifu" wa DRC kwa "miongo mitatu" na "kutoweza kurejesha mamlaka katika eneo lote.”
Alidai kuwa angalau makundi tisa yenye silaha, ikiwa ni pamoja na M23, tayari walikuwa wamejiunga naye katika mradi wake wa "Congo River Alliance" wa "umoja wa kitaifa na utulivu" wa DRC.
Kisha miaka kadhaa ya utulivu, waasi wa M23 ("March 23 Movement") walichukua tena silaha mwishoni mwa 2021 na kuteka maeneo makubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, na kusababisha watu zaidi ya milioni moja kukimbia, kulingana na Umoja wa Mataifa.