Ramadhan Kibuga
TRT Afrika, Bujumbura, Burundi
Dkt Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2018 akiwa na umri wa miaka 68 amejitosa kuwania urais nchini mwake DRC katika uchaguzi uliopangwa Disemba 20. Anasema lengo lake ni ''kuwarudishia raia wa Congo hadhi na haki zao.''
Kazi yake ya kuwatibu na kuwahudumia wanawake hasa waliofanyiwa ubakaji na ukatili wa kijinsia Mashariki mwa Congo ndiyo iliyompa jina maarufu la ''Daktari anayetengeneza wanawake.''
Binafsi Dkt Mukwege alihuzunishwa sana na hali hiyo: ''Wanawake wanapigwa, wanabakwa, wanapata majeruhi ya risasi, viungo nyeti kukatwakatwa, ukatili huo umekuwa unatumiwa kama silaha katika vita,'' aliandika Dkt Mukwege katika kitabu chake alichokiita ''Nguvu ya wanawake.''
Maisha ya misukosuko
Dkt Denis Mukwege Mukengere alizaliwa Bukavu, Kivu Kusini tarehe mosi mwezi Machi mwaka 1955. Baada ya elimu ya msingi na upili kuifanyia nyumbani, alijiunga na Chuo Kikuu cha Burundi na kuipata Shahada ya Udaktari mwaka 1983 kabla ya kwenda Ufaransa kuongeza elimu na kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake. ''Mazingira na matukio mbalimbali ndio yalinifanya niwe mtaalamu wa majeraha ya ubakaji,'' anasema.
Mbali na shughuli ya udaktari, Mukwege ni mchungaji katika dhehebu la Kiprotestanti Kanisa la Bukavu. Kazi hii ya wito wa kidini aliirithi kutoka kwa baba yake ambae pia alikuwa mchungaji.
Aidha Dkt Mukwege anayo familia. Yeye pamoja na mkewe Mapando Kaboyo wamejaaliwa kuwapata watoto watano.
Mwanzo wa taaluma
Licha ya mshahara mnono nichini Ufaransa, Dkt Mukwege alirudi nyumbani na kuhudumu katika Hospitali ya Lemera Kivu Kusini kama daktari kiongozi.
Lakini machafuko ya mwaka 1996 yalishuhudia Hospitali hiyo ikiteketezwa. Dkt Mukwege alinusurika kifo huku wauguzi na wagonjwa wakipoteza maisha. Mukwege alilazimika kuchukua hifadhi fupi nchini Kenya.
Mwaka 1999, baada ya kupata ufadhili wa Shirika la Kihisani la Sweden, Dkt Mukwege alirudi katika mji wake wa asili wa Bukavu na kuanzisha Hospitali maarufu ya PANZI ambayo iliwapokea wanawake waliofanyiwa dhulma za kingono.
''Nilishawishika na matatizo wanayokumbana nayo kinamama wanapojifungua. Na shida ya kupata tiba. Mimba zilikuwa zinaishia kwenye kilio. Sehemu nyeti zinatiririka damu na kuvunda. Kwangu taalumu ilikuwa imeanza,'' anasimulia.
Dkt Mukwege alilazimika kwenda kusoma zaidi Ufaransa na Ubelgiji hasa upasuaji wa fistula na kumfanya kuwa mmoja wa madaktari bingwa duniani wa taaluma hiyo.
Tangu kuasisiwa mwaka 1999, Hospitali ya PANZI iliobatizwa ''Kliniki ya Ubakaji'' imewatibu kinamama zaidi ya elfu 60. "Ubakaji unahusu marika yote. Wanawake, wasichana hata watoto wachanga. Mtoto mdogo niliyemfanyia upasuaji alikuwa na miezi sita na mzee zaidi alikuwa na miaka 80,'' anasema.
Tarehe 25 Octoba, 2012 wakati akirudi nyumbani, Dkt Mukwege alishambuliwa mjini kati Bukavu. Mlinzi wake wa nyumba aliuwawa papo hapo na gari lake kuchomwa huku Dkt Mukwege akiwekwa kitanzi. Alinusurika tu kutokana na wapita njia. Kwa mara nyingine tena, Dkt Mukwege akalazimika kukimbia na kutafuta hifadhi mara hii nchini Ubelgiji.
Licha ya kurudi nyumbani Dkt Mukwege alikuwa anatishiwa maisha yake kila mara. Hivyo, anaishi chini ya ulinzi mkali ndani ya hospitali yake akilindwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa.
''Kazi yake inamtia hatarini maana kuna makundi mengi yenye silaha yalihusika na ukatili wa kingono. Wanahofia kwamba waathirika huwa wanafichua siri wanapofika hapo Panzi,'' alisema mwanaharakati Vincent Bahati.
Licha ya misukosuko hiyo, hâta hivyo kazi yake ilianza kuzaa matunda. Mwaka 2018, Dkt Denis Mukwege alitunukiwa Tuzo ya Nobel kwa juhudi zake za kukomesha ukatili wa kingono kama silaha ya vita. Na hii ni baada ya kujizolea tuzo mbalimbali kote duniani.
Safari ya Kisiasa
Lakini imekuwaje Daktari aliyeongoza harakati za tiba na upasuaji wa wanawake pamoja na kutetea haki zao kwa karibu miaka 40 anajikuta katika safu ya mbele ya kuwania urais?
Dkt Mukwege aliutetea uamuzi wake, ''Zaidi ya miaka 20 napaza sauti nikichagiza amani hapa nchini bila mafaanikio. Lakini hali ya kutoadhibu ndio yazidi kuendelea. Napeleka ujumbe kwa viongozi wa nchi yetu lakini wanashindwa kutatua matatizo. Ndio nimeona badala ya kuagiza, kumbe bora nichukue mambo mikononi. Nikaamua kusimama katika nafasi hii ya urais,'' alisema Dkt Mukwege.
Aidha, ilani ya Dkt Mukwege imejikita kwenye mambo matatu muhimu: -
-Kumaliza Vita
-Kumaliza Njaa
-Kumaliza Maovu
Ingawa ametilia maanani suala la maendeleo ya Congo na kupendekeza mambo mengi lakini Dkt Mukwege anaamini kwamba, ''Bila amani hamna mradi wowote wa maendeleo unaweza kufanyika.''
Amejenga mkakati mkubwa wa sekta ya ulinzi ikiwa ni pamoja na kuunda jeshi lenye nguvu na ujuzi na kuyaondoa mara moja majeshi yote ya kigeni yaliopo ndani ya ardhi ya DRC.
Safari hatari ya siasa
Kampeni yake imezua hamasa kubwa miongoni mwa wananchi kama mama huyu Alphonsine Zawadi kutoka mji wa Kisangani.
''Hii nchi imeumia sana. Huyu daktari bingwa ambae pia ni mchungaji ananipa imani kuwa atakuwa ni bora kuliko wagombea wengine. Na pia yeye hajaweka mikono yake katika fedha za serikali.''
''Nilishawishika na matatizo wanayokumbana nayo kinamama wanapojifungua. Na shida ya kupata tiba. Mimba zilikuwa zinaishia kwenye kilio. Sehemu nyeti zinatiririka damu na kuvunda. Kwangu taalumu ilikuwa imeanza."
Wadadisi wa siasa za Congo wanahofia kwamba kujitosa kwake kwenye nafasi ya kuwania urais itahatarisha maisha yake.
' Mara hii maadui wake sio pekee wahusika wa ubakaji, lakini pia wanasiasa ambao watamuona Dk Mukwege kama tishio katika maslahi yao,'' anasema mdadisi Albert Ntumba.
Hofu nyingine ni uwezo na bahati yake ya kuweza kushinda uchaguzi wa Disemba 23 hasa ikizingatiwa kwamba hana chama maarufu katika ngazi ya taifa au mafungamano na wanasiasa.
Kwenye kampeni yake, Dkt Denis Mukwege anaungwa mkono na Vuguvugu la wasomi la ARCN (Alliance des Congolais pour la Refondation de la Nation)[Muungano wa wakongomani kwa ajili ya Ujenzi mpya wa Taifa] pamoja na Muungano wa Mashariki ya Kiraia maarufu 'Appel Patriotique' (Wito wa Uzalendo). Hao waliweza kukusanya dola laki moja na kumkabidhi Dkt Mukwege kama ya ada ya dhamana ya Uchaguzi wa Disemba 20, 2023.
Christian Moleka ni mdadisi wa masuala ya siasa za Congo, anasema, "Ukosefu wa Chama chenye mizizi na ngome ya kisiasa ni changamoto kwake. Lakini pia uwezo wake wa fedha ni mdogo ukilinganisha na wagombea wengine. Hivyo itamlazimu ategemee kura sana upande wa nyumbani Bukavu na pengine eneo la Mashariki ambako ni maarufu sana. Na hii pengine isitoshe kumpa ushindi katika uchaguzi wa Congo uliopangwa kufanyika Disemba, 20.''