Mgombea urais Denis Mukwege wa DR Kongo, daktari maarufu wa maradhi ya wanawake na mshindi wa Nobel, amefanya mkutano wake mkubwa wa kwanza wa kampeni katika mji aliozaliwa siku ya Jumamosi tangu kampeni kuanza rasmi mnamo Novemba 19.
Mukwege ameahidi kukabiliana na ufisadi na migogoro iwapo atachaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi wa mwezi ujao.
Akiwahutubia wafuasi wake katika mji wa mashariki wa Bukavu, daktari huyo mashuhuri alisema atatumia mamlaka ya kisiasa "kukomesha vita, kukomesha njaa" na kupambana na ufisadi.
"Ndani ya muhula wangu wa miaka mitano wa utawala, [nitakwenda] kuwarudishia watu wa Kongo utu wao, haki zao," alisema, akikosoa utegemezi wa nchi hiyo kwa misaada ya kigeni, ikiwa ni pamoja na msaada wa kijeshi wa kigeni.
"Leo hii wizi umekuwa ni jambo la kawaida nchini Kongo, ni jambo la kawaida kufanya matendo ya kifisadi," alisema daktari huyo mwenye umri wa miaka 68.
Mukwege alianzisha hospitali na wakfu wa Panzi katika eneo lenye migogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kushuhudia majeraha na magonjwa ya kutisha yaliyowapata waathiriwa wa ubakaji.
"Kimataifa, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha wanajeshi wa kigeni wanaondoka ardhi ya Kongo, na kwamba watu wa Kongo wajifunze kuwajibika kwa usalama wao wenyewe," Mukwege alisema.
Mnamo 2018, alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel pamoja na mwanaharakati wa Yazidi Nadia Murad kwa juhudi za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia kama silaha ya vita.
Aidha, mnamo mwezi Oktoba, Daktari huyo aliwasilisha nia yake ya kugombea urais akimaliza miezi kadhaa ya uvumi kuhusu mipango yake ya kisiasa.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, taifa maskini ambalo pia linakumbwa na mizozo katikati mwa Afrika, na lenye takriban watu milioni 100, linatarajiwa kufanya uchaguzi wa rais na wabunge tarehe 20 Disemba.
Makumi ya makundi yenye silaha yamekita mashariki mwa DRC, urithi wa vita vya kikanda ambavyo vilipamba moto katika miaka ya 1990 na 2000.
Mojawapo, ya makundi hayo, M23, limeteka maeneo mengi katika eneo hilo tangu lianzishe mashambulizi mwishoni mwa 2021, na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu na zaidi ya watu milioni moja kufukuzwa makwao.
Mashariki mwa Kongo pia ni makazi ya vikosi vya jeshi la kigeni, ikiwa ni pamoja na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa mataifa mbalimbali, na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliwapeleka wanajeshi nchini humo.