Uchaguzi DRC 2023: Tume ya Uchaguzi yapambana dakika za mwisho kufikisha vifaa vya kupigia kura

Uchaguzi DRC 2023: Tume ya Uchaguzi yapambana dakika za mwisho kufikisha vifaa vya kupigia kura

Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC-CENI imesema kila kitu kitakuwa sawa ifikapo Disemba, 20 ambayo ndio siku ya uchaguzi nchini humo.
Zaidi ya raia milioni 40 nchini DRC wanatarajiwa kupiga kura Disemba 20 kuchagua viongozi mbalimbali. 

Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya uchaguzi wa DRC utakaofanyika Disemba 20. Wakati huo huo, muda unaenda kwa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo CENI kuhakikisha imepeleka vifaa vya uchaguzi katika maeneo yote ya taifa hilo kubwa ambalo mpaka sasa baadhi ya maeneo yanakabiliwa na migogoro ya kijeshi.

Mkoa wa Ituri, mashariki mwa nchi, ni moja mwa maeneo yalioko mbali na ambayo yanakumbwa na machafuko ya mara kwa mara. Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi CENI imehakikisha kwamba kila kitu kitakuwa sawa ifikapo Jumatano.

Kufuatia usaidizi wa vifaa na ufundi wa Monusco, Tume ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa, asilimia 99 ya vifaa vya uchaguzi vimekwishawasilishwa kwenye makao makuu ya wilaya za Ituri, kulingana na Tume ya Uchaguzi CENI. Ni pamoja na maeneo yenye ushawishi mkubwa wa wanamgambo walio karibu na Serikali katika maeneo ya Ndjugu, Mahagi na Aru.

''Ni wanamgambo wakongomani na hao wanamgambo wana haki ya kuchagua. Waliruhusu tufanye uorodheshwaji wa wapiga kura. Tulizungumza na wakuu wa vijiji, waliruhusu pia tufanye kazi bila tatizo. Na hao hao wanamgambo walikubali tupeleke vifaa kwa ajili ya uchaguzi,'' alifafanua Jimmy Anga, Katibu mtengaji wa Tume ya CENI katika mkoa wa Ituri.

Hali tete Ituri Magharibi

Hali si shwari katika maeneo ya magharibi mwa Ituri. Maeneo ya Irumu, Mambassa na Oicha yanashuhudia waasi wa ADF wanamgambo kutoka Uganda ambalo kundi la Daesh.

''Kuna tatizo kubwa. Kunahitajika juhudi zaidi. Lakini hiyo ni shughuli iko chini ya himaya ya viongozi wa kijeshi wa mkoa. Tulisikiza kwa makini hutuba ya Gavana wa Kijeshi wiki iliopita. Alihakikisha kwamba katika maeneo yote, wapiga kura watakuwa kwenye vituo tarehe 20 Disemba,'' kwa mujibu wa Deogratias Bungamuzi, Kiongozi wa Baraza la mkoa la vijana katika mkoa wa Ituri.

Shughuli ya kupeleka vifaa katika mikoa wa Kivu Kaskazini na Kivu Kusini pamoja na mkoa wa Ituri inaendelea. Mapema Kati ya mwezi wa Aprili na Mei, Umoja wa Mataifa walisafirisha tani 128 za vifaa vya uchaguzi. Na kuanzia tarehe 5 Disemba, ndege za Monusco zilisheheni vifaa vya ziada sawa tani 127. Ni pamoja na mashini za uchaguzi na nyaraka za kupigia kura.

Ndege za Misri

Ili kuokoa muda, Serikali ya Congo kwa upande wake, imetangaza mwishoni mwa juma kuwasili kwa ndege 2 za kijeshi za Misri aina ya Hercules C-130 ili kusaidia usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi katika maeneo mbalimbali.

Ndege hizo zitasaidiana na ndege za Jeshi la Congo FARDC pamoja na helikopta za Monusco.

Ndege hizo zilizoazimwa kutoka jeshi la Misri zinafahamika sana na wataalamu kwa uwezo wake wa kutumika katika mazingira mbalimbali. Lakini pia sifa yake kubwa ni uwezo wa ndege hizo wa kupaa na kutua katika viwanja vidogo au viwanja ambavyo havikuandaliwa vizuri. Na hii itasaidia hasa kupeleka vifaa kwenye maeneo mbalimbali ya DRC.

Hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu, ndege hizo mbili hazitoshi. Lakini serikali imewapa raia matumaini kwa kusema kuwa Jeshi la anga la Congo litatumia uwezo wake kukidhi mahitajio ya Tume Huru ya Uchaguzi CENI.

Kuhusu mikoa mingine, Tume ya Umoja wa Mataifa imesema iko kwenye mazungumzo na Tume ya Uchaguzi ili waeleze mahitaji mahususi katika usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi kwenye maeneo mbalimbali ya DRC.

Tazama: Raia wa Afrika Mashariki wana maoni gani kuhusu uchaguzi wa DRC?

TRT Afrika