Lissu alipata zaidi ya 51% ya kura zilizopigwa kumpa ushindi wa Uenyekiti wa chama Kitaifa / Picha: Tundu Lissu 

Tundu Antipas Lissu ndoye mwenyekiti rasmi wa CHADEMA taifa.

Lissu alitangazwa mshindi alfajiri Jumatano, Januari 22, baada ya shughuli ya upigaji kura uliofanyika usiku kucha katika mkutano wa wajumbe wa taifa wa chama hicho, jijini Dar es Salaam.

''Ushindi huu ni wetu sote!'' aliandika Lissu katika ukurasa wake wa X muda mfupi baada ya matokeo kujulikana.

Katika mkutano huo huo, John Heche alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Taifa baada ya kukusanya zaidi ya 57% ya kura.

Mwenyekiti anayeondoka FreemanMbowe alikuwa wa kwanza kukubali matokeo ya kura hizo na kumpongeza mshindani wake.

''Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama chetu CHADEMA uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025,'' alisema Mbowe. ''Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la Uongozi wa Chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele Chama chetu.

Chadema Party

Freeman Mbowe amekuwa mwenyekiti wa CHADEMA TAIFA tangu Septemba 14, 2004. Anasifiwa kwa mabadiliko mengi yaliyotokea ndani ya chama kwa miongo miwili iliyopita, na kuahidi kuleta zaidi iwapo ataendelea kukitumikia chama kama mwenyekiti wake wa taifa.

TRT Afrika