Na Deogratius Temba
Serikali ya Tanzania, ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, sura ya 366, ambapo moja ya kifungu cha sheria hiyo kinachoangaziwa ni pamoja na kuongezwa kwa muda wa likizo kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti.
Kulingana na kifungu hicho, mama aliyezaa mtoto njiti ataendelea kuwa likizo ya malipo hadi kutimia kwa wiki 36 za ujauzito na kisha aendelee na likizo yake ya uzazi kama kawaida.
Katika muswada huo, marekebisho yanafanyika kwenye sheria ya msingi ya awali kwamba: Kifungu cha 33 cha muswada kinaeleza kwamba“ Sheria inarekebishwa katika kifungu cha 33 kwa- (a) kuongeza mara moja baada ya kifungu kidogo (7) yafuatayo: "(8) Mfanyakazi anayezaa mtoto kabla ya muda wake ana haki ya likizo ya uzazi inayolipiwa kuanzia tarehe ya kujifungua hadi kukamilika kwa wiki thelathini na sita za ujauzito na hadi kipindi cha likizo ya uzazi kilichotolewa chini ya kifungu kidogo (6) katika mzunguko wa likizo.";
Inaelezwa kwamba, lengo la marekebisho haya ya sheria, sio upendeleo tu kwa wanawake, bali unalenga kulinda ustawi wa afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na kuhitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa baba na mama.
Mtandao wa Haki ya Afya ya Uzazi (SRHR), unaoratibiwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT-T) unapendekeza uwepo wa likizo ya kutosha kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanapata nafasi ya kumlea mtoto njiti bila tatizo.
SRHR, wakiongozwa na Taasisi ya Doris Mollel, Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) wanadai kuwa, ili kuongeza tija katika uzalishaji mali nchini na kujenga taifa la watu wenye afya njema ni muhimu kulinda afya na ukuaji wa watoto njiti.
“Kifungu kina tija kwa wafanyakazi waliojifungua kabla ya muda ili kuruhusu mzazi kuhudumia mtoto kwa ukaribu ili atengemae isipokua siku zilizotajwa hapo ziongezeke kutoka wiki 36 mpaka wiki 40 kwa sababu za kiafya hasa makuzi ya mtoto,” linasema moja ya pendekezo la Mtandao huo kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii waliowasilisha kuhusu muswada huo.
Kwa upande wao SHRSR na TUCTA, wanapendekeza kuwa malipo ya wiki za kabla ya kujifungua ambazo mama angekuwa hajajifungua ziongezeke hadi wiki 40 kwani wanawake wengi hujifungua kati ya wiki ya 36 hadi 40 na ndipo ianze likizo rasmi ya uzazi.
Likizo inayopendekezwa ni kwa wanawake (Mama anayejifungua) na mume wake kwasababu za msingi ambazo ni kwamba, mtoto njiti anahitaji malezi ya pande zote na pia mama aliyejifungua anahitaji usaidizi wa mwenza wake wakati huu.
Kwa mujibu wa sheria kuu ya ajira na mahusiano kazini nchini Tanzania, sura ya 366, vifungu 33 na 34 vinavyozungumzia likizo za watumishi, hakuna kabisa suala la likizo ya mama anayejifungua mtoto njiti, lakini kutokana na marekebisho haya, kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa imegusia suala la mtoto njiti kwenye sheria.
Mfumo bora kwa watoto njiti
Jambo la msingi la la kiafya kwa mtoto aliyezaliwa njiti, ni kutunzwa kwa mfumo wa Kangaroo, ambao huusisha mama kumbeba na kumuwekwa kifuani mtoto wake aliyezaliwa chini ya miezi tisa na kumfanya kuwa na mawasiliano ya kimwili ya moja kwa moja na mzazi wake, badala ya matumizi ya mashine maalumu ambazo gharama za huduma zake ni kubwa.
Gharama za hospitali zilikuwa kubwa sana ambapo kwa siku tulitakiwa kulipa Dola za Kimarekani 79…hata hivyo tulishauriwa kuondoka Hospitalini na tukatumia mfumo huu wa kangaroo, ambapo mimi kama baba, nililazimika kumsaidia mke wangu kumweka mtoto kifuani ili apate joto la mzazi
Mfumo wa Kangaroo ulipendekezwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1978 na madaktari wa watoto wawili katika kitengo cha uzazi katika Hospitali ya San Juan de Dio huko Bogotá, Colombia.
Hata leo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lina imani na njia hiyo.
Mohamed Saleh, ni mume wa Saada Nassor Mohamed, wakazi wa Dar es salaam nchini Tanzania ambaye amezaa watoto wawili kabla ya muda (njiti).
Mohamed anaeleza namna avyowajibika kumsaidia mke wake katika malezi ya mtoto njiti ili kukoa maisha ya mtoto lakini pia kupunguza gharama ambazo zingelipwa hospitalini.
“Gharama za hospitali zilikuwa kubwa sana ambapo kwa siku tulitakiwa kulipa Dola za Kimarekani 79…hata hivyo tulishauriwa kuondoka Hospitalini na tukatumia mfumo huu wa kangaroo, ambapo mimi kama baba, nililazimika kumsaidia mke wangu kumweka mtoto kifuani ili apate joto la mzazi,” anasema.
Ilimlazimu Mohamed asitishe shughuli zake za kujiingizia kipato ili abaki nyumbani na kumsaidia mke wake.
“Wakati tunaruhusiwa kutoka Hospitalini tulipewa masharti endapo tunataka mtoto apone, basi, asishikwe na mtu mwingine yeyote isipokuwa mimi na mama yake.”
“Nafasi ya baba ni muhimu sana ili kuwa na mtoto mzuri mwenye afya njema. Mwanaume akishiriki kumtunza mtoto ataokoa gharama za matibabu, kwa sababu mtoto hatopatwa na maambukizi,” anaongeza.
Watoto njiti wanaweza kuishi, kushamiri na kubadili dunia , lakini kila mtoto lazima apata fursa ya kuishi. Kulingana na muongozo huu, siha ya watoto njiti sio suala la kiteknolojia tu bali pia kuhakikisha kuwa fursa ya huduma muhimu za afya ambazo zinakwenda sanjari na mahitaji ya familia
Saada bado anakumbuka namna alivyoshtuka baada ya kukabidhiwa mtoto wake mara baada ya kujifungua.
“Nilishtushwa na umbo dogo la mtoto, nilimuuliza daktari kama alikuwa amenibadilishia mtoto…nilimuita mume wangu na kumweleza,” anaeleza.
Kukubaliana na hali halisi
Mara baadaye kueleweshwa vizuri na daktari kuhusu hali ya mtoto wake, Mohammed na mkewe waliazimia kutumia pamoja mfumo wa Kangaroo, wakiamini ndi njia pekee ya kumuokoa mtoto wao.
Dharura ya afya ya umma
Kwa mujibu wa WHO watoto njiti ni suala la dharura la afya ya umma.
Kila mwaka, inakadiriwa kuwa watoto milioni 15 huzaliwa kabla ya wakati, ikiwa ni zaidi ya mtoto 1 kati ya 10 ya watoto wote wanaozaliwa duniani, na idadi kubwa zaidi ya watoto milioni 20 huzaliwa wakiwa na uzito mdogo.
Nilishtushwa na umbo dogo la mtoto, nilimuuliza daktari kama alikuwa amenibadilishia mtoto…nilimuita mume wangu na kumweleza
Idadi hii huongezeka huku watoto wanaozaliwa njiti wakichangia pakubwa sababu kubwa ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5.
Muongozo mpya
Novemba 2022, WHO ilizindua muongozo wa kuboresha uhai na matokeo ya kiafya ya watoto wanaozaliwa njiti kabla ya wiki 37 au wenye uzito wa chini ya kilo mbili na nusu wakati wa kuzaliwa.
Muongozo huo unasisitiza mfumo wa Kangaroo kuanza kutumika, pindi tu mtoto anapozaliwa.
“Watoto njiti wanaweza kuishi, kushamiri na kubadili dunia , lakini kila mtoto lazima apata fursa ya kuishi. Kulingana na muongozo huu, siha ya watoto njiti sio suala la kiteknolojia tu bali pia kuhakikisha kuwa fursa ya huduma muhimu za afya ambazo zinakwenda sanjari na mahitaji ya familia,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.