Kila ifikapo tarehe 2 ya mwezi wa nne, Dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usonji. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kuwezesha Sauti za Usonji’./Picha: Wengine

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Grace Anna Lyimo hakuona kasoro yoyote wakati mtoto wake anazaliwa.

Hata hivyo, mabadiliko madogo yaliyoanza kujitokeza kwa Erick yalianza kumshtua na kumtia wasiwasi.

"Haikuwa rahisi kung’amua ni kitu gani kilichokuwa kinamsumbua Erick, lakini kukosa utulivu nyakati za kunyonya ndicho kilichonishtua zaidi, halikuwa jambo la kawaida,” Grace anaelezea TRT Afrika.

Kama mzazi mwingine, Mama Lyimo aliamua kumpeleka mwanaye kwa wataalamu ya afya.

Ilikuwa ni mfululizo wa safari kwa wataalamu wa magonjwa ya watoto baada ya nyingine, kwa mama huyu mzaliwa wa Kibosho, mkoani Kilimanjaro, nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mtoto mmoja kati ya 100 ulimwenguni, wanakabiliwa na Usonji. Hii ni hali ya kibaiolojia anayoipata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea./Picha: CAT

“Awali, niliambiwa kuwa hali ile ilikuwa ni ya mpito tu na kuwa ipo siku itakwisha kadiri mtoto anavyoendelea kukua,” anaendelea kusema.

Hata hivyo, hali iliendelea kuwa hivyo hivyo kwa mtoto Erick, hata alipofikisha umri wa miaka mitano, hatua iliyomlazimu mama huyo mwenye watoto wanne, kusafiri mpaka Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya kusaka matibabu sahihi kwa mwanaye.

Hata akiwa huko, jibu likawa ni lilelile, kuwa 'hali hiyo itaisha kadiri mtoto anavyokuwa.'

“Hata hivyo, walinishauri nimtafute mtaalamu wa ndimi atayeweza kumsaidia mwanangu katika matamshi yake,'' anakumbuka.

Mama Lyimo aliamua kwenda katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), kumtafuta mtaalamu huyo, bila mafaniko yoyote.

Grace Anna Lyimo akiwa katika moja ya semina zilizoandaliwa na Connect Autism Tanzania (CAT)./Picha: CAT

Kama mzazi aliyekuwa tayari kupambania afya ya mwanaye, Mama Lyimo alifika hadi Afrika Kusini kwa ajili ya tiba ya Erick.

Hatua hii ilimlazimu kuacha kazi iliyokuwa inamuingizia kipato kizuri katika hospitali ya Aga Khan, ili aweze kutenga muda zaidi kwa ajili ya afya ya mwanaye.

"Kwa wakati ule, Erick alihitaji matibabu na uangalizi mkubwa, hivyo sikuwa na budi ila kuacha kazi iliyoniingizia mshahara mzuri tu,” anaambia TRT Afrika.

Kukosa fursa ya kusoma

Erick alikosa fursa ya kupata elimu kutokana na hali yake.

Kulingana na Mama Lyimo, hakuna shule iliyokuwa tayari kumpokea Erick kutokana na kuwa na hali ya Usonji aliyokuwa nayo.

"Nami sikukata tamaa, nilizunguka mkoa mzima wa Arusha, nikitafuta shule sahihi kwa ajili ya Erick, bila mafanikio yoyote,” anaelezea Mama Lyimo.

Usonji ni ugonjwa unaokumba ubongo na kusababisha mtoto au mtu mzima kushindwa kuhusiana na watu wengine na wakati mwingine kushindwa kushiriki ipasavyo katika shughuli za kijamii. /Picha: CAT

Vitisho vya Kuawawa

Erick alikumbana na unyanyapaa na vitisho vya kuuwawa kutokana na hali yake.

Kulingana na mama yake, wapo waliodiriki kutaka kuutoa uhai wa Erick, wakihusisha hali yake na mambo ya kishirikina.

"Erick alitengwa na jamii kutokana na hali yake, niliumia sana kuona akinyanyapaliwa na jamii iliyomzunguk. Hali hiyo ilinipa ari ya kufanya jambo ili niweze kuielimisha jamii nzima kuwa Usonji si laana wala ushikirina, bali ni hali ya kibaiolojia tu,” anaambia TRT Afrika.

Kuanzishwa taasisi ya CAT

Kwa kuguswa na changamoto ya Erick, na akisukumwa na ari ya kubadilisha kasumba ya jamii nzima kuhusu Usonji, ilipofika mwaka 2015, Mama Lyimo alianzisha taasisi isiyo ya kiserakali iitwayo Connect Autism Tanzania (CAT) ikiwa na lengo la kuwasaidia watu, haswa watoto waishio na hali hiyo.

Taasisi ya CAT husaidia makundi hayo kupitia kuwajengea uwezo, kufanya utetezi, kuongeza uelewa wa jamii na kuwatafutia fursa watu wenye kuishi na hali ya Usonji.

Mama Lyimo alianzisha taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Connect Autism Tanzania (CAT) ikiwa na lengo la kuwasaidia watu, haswa watoto waishio na hali hiyo./Picha: CAT

Taasisi ya CAT inasaidia makundi hayo kupitia kuwajengea uwezo, kufanya utetezi, kuhamasisha jamii na kuwatafutia fursa za kiuchumi watu wanaoishi na hali ya Usonji.

“Siku zote, tumekuwa tukipambana kuhakikisha kuwa watu hasa watoto waishio na Usonji wanashirikishwa kwenye mambo mbalimbali kwenye jamii, kama vile kupata elimu kama watu wengine wa kawaida na kufanya shughuli za kuwaingizia vipato,” anasema.

Toka kuanzishwa kwake, taasisi hiyo imeendesha semina na warsha kwa wanafamilia, walimu, watumishi wa serikali, maafisa maendeleo ya jamii hata vyombo vya dola kwa lengo la kuongeza uelewa wa hali ya Usonji na kuondoa unyanyapaa kwa watu wenye hali hiyo.

"Nia yetu ni kuona kuwa watu wenye Usonji wanashirikishwa, hali hairidhishi kwani kasi ni ndogo sana, wazazi na walezi hawajaamini kuwa watoto wa aina hii wanaweza kutangamana na wale wengine wa kawaida," anasema Grace.

Kulingana na Mama Lyimo, taasisi ya CAT imeanza na watoto 17, katika mchakato wa kuwapa elimu, kuwafundisha namna ya kupata huduma za usafiri na namna ya kufanya shughuli za kujiingizia kipato.

"Ndani ya miezi michache tu, watoto hawa wamejisikia kama sehemu ya familia kwani wanafanya kazi kama watu wengine, hata baadhi yao wanajitegemea wakati wengine wamapata ajira," anaelezea.

Mama Lyimo anasema kwa sasa, serikali imeanza kutambua umuhimu wa kuwajengea uwezo watu kutoka makundi hayo.

Ushirikishwaji wa kijamii ni jambo la msingi sana, ni muhimu kuwachanganya watu wenye ulemavu wa akili na makundi mengine katika jamii

Mama Lyimo

Licha ya kuwa uwiano unapaswa kuwa 1:5, yaani mwalimu mmoja ahudumie watoto watano wenye usonji, hali ni tofauti sana kwa Tanzania.

Kwa mujibu wa Mama Lyimo, hali si ya kuridhisha kwani mwalimu mmoja analazimika kufundisha watoto wote, wenye hali ya kawaida na wale wenye ulemavu wa akili kwa wakati mmoja.

Japo anaridhishwa na utayari wa serikali kwenye suala hili.

Inaridhisha kuona kuwa serikali imetoa utaratibu wa kuwepo mwalimu wa elimu maalumu kwenye ila wilaya nchini Tanzania. Serikali inasisitiza kuwa watoto wenye ulemavu wa akili lazima waandikishwe shule, jambo hili linatia moyo sana.

Mama Lyimo
Licha ya kuwa uwiano unapaswa kuwa 1:5, yaani mwalimu mmoja ahudumie watoto watano wenye usonji, hali ni tofauti sana kwa Tanzania./Picha:LITAFO

Mitaala ya Elimu isiyojali wenye Usonji

Hata hivyo, ni masikitiko kwa Mama Lyimo kuona mitaala kwenye taasisi nyingi za elimu hazijaweka mazingira mazuri kwa watoto wenye Usonji.

Hali hii, kulingana na Mama Lyimo inawalazimu wazazi wengi kuwaficha watoto wao kwa hofu ya kudhihakiwa na kunyanyapaliwa na jamii.

“Inasikitisha kuona bado mifumo yetu ya elimu sio shirikishi na haijaweka msisitizo kwa watu kutoka kundi hili,” anaweka wazi.

Kulingana na Mama Lyimo, taasisi ya CAT imezunguka maeneo mengi ya nchini Tanzania kujaribu kuhamasisha juu ya umuhimu wa elimu shirikishi kwa watu wenye Usonji.

“Shirika letu limekuwa linatoa mafunzo juu ya elimu jumuishi kwa watoto wenye mahitaji maalum na suala zima la watu wenye ulemavu katika ngazi mbalimbali ikiwemo kwa viongozi wa serikali tumekuwa tukiwafundisha suala la watu wenye ulemavu na mazingira yao.”

Mama Lyimo anasema kuwa jamii inahitaji kuwa na elimu jumuishi kwa lengo la kuwaweka watu katika usawa na kutoa fursa sawa kwa watu wenye mahitaji maalumu au watu wenye ulemavu.

Mama Lyimo akizungumza na aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini  Gabriel Fabian Daqarro kuhusu namna wanavyowasaidia watoto wenye Usonji./Picha: CAT

Mama Lyimo anasisitiza kuwa elimu jumuishi ni njia moja wapo ya kupunguza utegemezi katika jamii hususani kwa watoto wenye mahitaji maalumu.

Ukubwa wa Tatizo

Kulingana na Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania, Dkt Godwin Mollel tatizo la Usonji linaendelea kuongezeka ndani ya nchi hiyo na duniani kwa ujumla, huku akisema kuwa kwa mwaka 2021 katika kila watoto 44 mtoto mmoja alikuwa na changamoto ya Usonji, wakati kwa mwaka 2023 katika kila watoto 36, kila mtoto mmoja alipatikana na Usonji.

Aidha, Dkt Mollel amesema, watoto wenye changamoto ya Usonji wanatakiwa uangalizi wa karibu na kukuza vipaji vyao vya uvumbuzi, ili kuleta tija katika jamii.

Kuna wanasayansi wakubwa Duniani ambao wamegundua mambo mbalimbali na binadamu wakayafurahia, baadhi yao walikuwa watoto wenye changamoto kama hii ya Usonji

Dkt Mollel

Kila ifikapo tarehe 2 ya mwezi wa nne, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usonji, huku kauli mbiu ya mwaka 2024 ikiwa ni ‘Kuwezesha Sauti za Usonji’.

Baadhi ya watu maarufu wanaosadikiwa kupata hali ya Usonji katika maisha yao ni pamoja na Elon Musk na Bill Gates, pamoja na wataalamu wa muziki Beethoven, Mozart na mwanasayansi anayedhaniwa kuwa na akili nyingi, Albert Einstein.

TRT Afrika