Tanzania imepitisha jina la Dkt Faustine Ndugulile kuwania nafasi ya ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kanda ya Afrika.
Dkt Ndugulile anakuwa muafrika mashariki wa kwanza kuwania nafasi hiyo ya juu ya kikanda ambayo inalenga kukuza mashirikiano na ushiriki wa vijana na wanawake katika masuala ya afya duniani.
Katika taarifa yake, Dkt Ndugulile aliahidi kuwa kiongozi ambaye atawezesha nchi za Afrika kutengeneza mustakabali wa afya.
"Ninalenga kuboresha afya na ustawi wa jumla wa wakazi wa Afrika," alisema katika taarifa yake kwa Waziri wa Afya wa Tanzania.
Kwa sasa, nafasi hiyo inashikiliwa na raia wa Bostwana, Dkt Matshidiso Moeti, ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.
Dkt Ndugulile ni nani?
Akiwa na taaluma ya udaktari, Dkt Ndugulile amebobea katika afya ya umma. Aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, kabla ya kuhamishiwa kwenda Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kwa sasa, Dkt Ndugulile ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na pia ni mbunge wa jimbo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.