Visa vya kipindupindu, ugonjwa unaosababishwa na maji machafu, vimeongezeka maradufu katika nchi 10 za Afrika, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni.
WHO iliripoti kuwepo kwa wagonjwa zaidi ya 26,000 na vifo 700 katika wiki nne za mwanzo wa mwaka 2024, idadi ambayo inaongeza mara mbili ya takwimu zilizoripotiwa mnamo 2023 katika kipindi kama hicho.
‘’Wagonjwa wa kipindupindu wanaongezeka duniani kote, na kumekuwa na ongezeko kubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa barani Afrika, mashariki na kusini mwa Afrika zimeathiriwa vibaya sana,’’ ameonya Dk. Fiona Braka, Kiongozi wa Timu ya WHO Kanda ya Afrika, Operesheni za Dharura, katika taarifa.
Zambia, Zimbabwe, Msumbiji, Tanzania, DRC, Ethiopia, na Nigeria zinakabiliwa na "milipuko," na kuna hatari kubwa ya kuenea zaidi, imesema WHO.
Mabadiliko ya tabianchi
Dk. Braka amesema rekodi za sasa za kipindupindu ''zitaongezeka kwa sababu tu watu hawana huduma ya maji safi na vyoo.''
Kuongezeka kwa mafuriko yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa ugonjwa huo, ambao huenea baada ya kutumika kwa chakula au maji yaliyochafuliwa.
Vimbunga na ukame vimepunguza upatikanaji wa maji safi, na hivyo kutengeneza mazingira bora ya kipindupindu kustawi.
Mwaka jana, kimbunga kilisababisha mlipuko nchini Msumbiji, na kurekodi zaidi ya wagonjwa 4000 na vifo 131.
Pia mnamo 2023, mvua kubwa na mafuriko yaliathiri Zambia, na kusababisha milipuko.
WHO inasema inaunga mkono juhudi zote za chanjo katika nchi zilizoathirika, huku Zambia ikichanja zaidi ya watu milioni 1.7 na Zimbabwe ikilenga kutoa chanjo kwa watu milioni 2.3 ifikapo mwisho wa mwaka.