Kisukari au Diabetes ni ugonjwa ambao siku hizi umekuwa ukisikika mara kwa mara. Tofauti na miaka iliyopita ambapo ugonjwa huu, ulikuwa ukinasibishwa na watu wenye umri mkubwa, hivi sasa, takwimu za afya zinaonyesha ugonjwa huu umekuwa hatari zaidi na hata kuathiri watoto wadogo.
Shirika la Afya Duniani-WHO linasema kuna zaidi ya watu milioni 24 barani Afrika ambao wanaishi na ugonjwa huu ambao una athari mbalimbali za kiafya kwa mwanadamu.
Wataalamu wa afya wanasema, kumekuwa na ongezeko la ugonjgwa wa kisukari kwa sababu ya mabadiliko ya mfumo wa maisha.
"Mtu unatoka nyumbani asubuhi kwenye gari, ukifika kazini unakaa, kutoka kazini kwenye gari, tena nyumbani ukifika unakula na kukaa," anaelezea Dk. Elisha Osati, mtaalamu wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Muhimbili, Tanzania.
Ugonjwa wa kisukari una madhara makubwa, miongoni mwao, ni pamoja na kusababisha upofu, figo kushindwa kufanya kazi, kupata mshtuko wa moyo, kiharusi au stroke na hata unaweza hata kusababisha mtu kukatwa viungo vya mwili.
"Vyakula tunavyokula vingi ni vya wanga, na mafuta hivyo kusababisha madhara mwilini," Dkt. Osati anaongeza.
"Unakuwa mwingi mwilini na ukizingatia watu hawafanyi mazoezi na hawajishighulishi. Na unywaji wa pombe umekuwa mwingi na wa kupindukia pamoja na uvutaji sigara," anasema.
Lakini Utajuaje kama una kisukari/Diabetes? Zifuatazo ni baadhi ya dalili zake.
-Kuhisi kiu sana
• Kuhitaji kukojoa mara nyingi zaidi kuliko kawaida
• Macho kutoona vizuri
• Kuhisi uchovu
• Kupunguwa uzito ghafla bila kukusudia
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu
Wataalam pia wanashauri kuwa ni vyema kuamua kujitahidi kufikia uzito unaofaa wa mwili.
• Kufanya mazoezi ya viungo kwa angalau dakika 30 za mazoezi ya wastani kila siku
• Kula chakula cha afya na kuepuka sukari na mafuta mengi.
• Kutovuta sigara.