Patience Achieng alipata maradhi ya kupooza akiwa na miaka 14 na kushindwa kutembea wala kuongea./Picha: Patience

Pauline Odhiambo

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Patience Achieng alikuwa na umri wa miaka 14 kabla ya kuugua ugonjwa wa kupooza uliomfanya kushindwa kuongea wala kutembea. Japokuwa ilimchukua wiki mbili kwa binti huyo kutoka Nairobi kuweza kuongea tena, lakini ilimchukua miaka mitatu kuweza kutembea.

"Ilinitokea wakati nikiwa katika mwaka wangu wa kwanza shule mwaka 2014. Nilienda kwenye kituo cha afya cha shule baada ya kuhisi homa. Walidhani ni Malaria, wakaamua kunipa dawa ili nipone," Patience, mwenye umri wa 24, anaiambia TRT Afrika.

Hata hivyo, wazazi wake waliamua kumpeleka hospitali baada ya afya yake kushindwa kuimarika.

Baada ya wiki mbili, Patience aliruhusiwa kutoka hospitali. Hata hivyo, afya yake ilizidi kuzorota ndani ya siku chache.

"Nilishindwa kuhisi miguu yangu nilipoamka siku moja asubuhi," anasema. "Sikuweza kuhisi mikono yangu, na nilishindwa kuzungumza. Nilipooza."

Vipimo toka hospitali vilionesha kuwa Patience alikuwa na uvimbe kwenye moyo wake, na hivyo kushindwa kusafirisha damu kwenye ubingi wake, na kupelekea hali ya kupooza.

Baada ya miaka 3, Patience alianza kujifunza kutembea baada ya kupooza. Picha: Patience

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna sababu nyingi zinazopelekea hali ya kupooza.

Kwa watoto wenye umri wa kati ya siku 29 hadi miaka 18, hali ya kupooza ambayo inahusishwa na matatizo ya moyo na seli mundu.

Athari nyingine ni kama magonjwa ya kuambukiza, kupata kiwewe, maumivu ya kichwa na matatizo kwenye mishipa ya damu.

"Daktari aliniambia kuwa nisingeweza kutembea wala kuzungumza tena kwa sababu ya hali ya kupooza niliyokuwa nayo, ilikuwa ni muujiza baada ya kuanza kutembea wiki mbili baadaye," anakumbuka Patience.

"Niliamka asubuhi moja na kumnong'oneza mama yangu, 'Unajua kuwa naweza kuzungumza sasa?' Kama ilivyokuwa hali ya kupooza, uwezo wangu wa kuzungumza ulirejea usiku. Hata daktari akashangaa."

Safari ya kupona

Patience alitumia vifaa mbalimbali vya kumuwezesha kutembea kama vile kiti cha magurudmu, kabla ya kuweza kujimudu mwenyewe.

Nia yake ya kutaka kutembea tena ilisukumwa na tamaa yake ya kutaka kuendelea na masomo yake ya Sekondari.

Shule nyingi hazikuwa tayari kumpokea, zikidai kuwa hazikuwa na miundombinu rafiki kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu.

"Pamoja na kwamba nilipambana ili nirudi shule, safari ya kukubalika kama mwanafunzi mwingine wa shule ilikuwa ni mtihani mwingine," anasema Patience, ambaye kwa sasa ameanzisha mradi wa kutengeneza sehemu za mpando kwa wanafunzi wenye ulemavu mashuleni.

Patience alijifunza kutembea tena baada ya kupooza kwa miama 3. Picha: Patience

"Nilikuwa bado nikitumia msaada wa kutembea, na ndipo nilipojua kuwa nina ulemavu huu. Familia yangu ilikuwa ikinisaidia kwa kila kitu wakati wote, lakini ilikuwa vigumu kukubali kwamba sasa nililazimika kutegemea wanafunzi wenzangu kwa usaidizi."

Ilimuwia vigumu kwa Patience kuweza kutoka nje ya darasa lake, kwani mguu wake wa kushoto na mkono ilikuwa dhaifu.

"Ingenichukua kiasi cha saa moja kuelekea darasani. Hata kuandika na kuchora ilikuwa ngumu kwa sababu sikuweza kutumia mikono yote miwili, walimu walishindwa kunivumilia kufuatia hali hiyo," anasema.

Baadhi ya wanafunzi waliopata kusoma na Patience walikuwa na roho nzuri. "Walinisaidia kujiandaa, walinisindikiza darasani, walikuwa nami kwa kila hatua," anasema.

Siku moja, akiwa amechoka kusaidiwa, Patience aliamua kutembea mwenyewe kuelekea darasani. Hata hivyo, alidondoka na kuumia mguuni. Akajaribu tena, na kufanikiwa kuingia darasani.

"Ilinibidi kufanya hivyo ili niweze kusikia furaha tena," anasema Patience, alihitimu mwaka 2019, na kujiunga na Chuo Kikuu.

Kwa sasa, Patience hatumii vifaa vyovyote wakati wa kutembea. Picha: Patience

"Kwa sasa situmii vifaa vya kutembea tena...ikiwa ninataka kusimama moja kwa moja, ni lazima nipinde mguu wangu wa kushoto. Vinginevyo niko sawa kabisa," anasema.

Afya ya Akili

Kitendo cha kushindwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu, kilimpa Patience sonona.

"Nilitamani kujiua, nilikuwa najiuliza, 'Kwa nini mtu ateseke hivi?' Kama bahati, wazazi wangu walinipeleka kwa mwanasaikolojia, aliyenisaidia kupona," anaiambia TRT Afrika.

Patience akaanza kuandika makala na kuzisambaza kwenye majukwaa ya kusaidia watu wenye ulemavu, na kuibua hamasa.

"Nilichoka kusubiri kukubaliwa na mfumo wa shule, hivyo nilielekeza nguvu zangu katika kuwasaidia watoto wadogo na vijana kujisikia kuwa wamejumuishwa na kulindwa," anasema Patience, ambaye sasa anafanya kazi na UNICEF na Gifted Community Centre jijini Nairobi.

"Shabaha yangu ni kwenye afya na ustawi wa akili kwa watoto waishio na ulemavu, kuwahakikishia kuwa zipo sera zinazolinda haki zao."

Patience anawasaidia watoto wenye ulemavu waweze kushirikishwa kwenye mambo mbalimbali. Picha: Patience
TRT Afrika