Rais wa Kenya William Ruto amezielekeza mamlaka za elimu nchini humo kufungua shule Mei 13, kufuatia kucheleweshwa mara mbili kutokana na mafuriko makubwa yaliyoikumba nchi hiyo.
"Wazazi wote wanashauriwa kuzingatia maelekezo ya idara ya hali ya hewa na yale ya serikali, kwa sasa ni salama zaidi kwani tumechukua hatua stahiki za usalama," amesema Rais Ruto.
Kulingana na Ruto, serikali ya Kenya, kupitia mfuko wa maendeleo wa jimbo, umekarabati madarasa na maeneo mengine muhimu ya kujifunzia na hivyo ni muhimu kwa shule zote nchini humo kufunguliwa Mei, 13, 2024.
“Ni muhimu kwa wazazi kuanza kuwaandaa watoto wao kwa ajili ya siku ya ufunguzi wa shule,” alisisitiza Rais Ruto.
Awali, serikali ya Kenya ilipanga Aprili 29, 2024 kama siku ya kufungua shule kabla kuamua kusogeza mbele mpaka tarehe 6, mwezi wa tano.
Takribani watu 257 wanahofiwa kupoteza maisha katika mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua za El Nino zilizoukumba ukanda wa Afrika Mashariki.