Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ICRC linasema kuwa msaada wa haraka wa kibinadamu unahitajika kutokana na tishio la mafuriko zaidi.
Mafuriko hayo yameharibu barabara nane muhimu katika eneo la Kaskazini Mashariki nchini Kenya.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Mashariki, John Otieno amewataka wakazi wa eneo hilo kujiepusha na maeneo yaliyokumbwa na mafuriko huku akisema kuwa eneo la Mandera ndilo lilioathirika zaidi huku likishuhudia vifo saba kufikia sasa.
Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema kuwa mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa katika barabara kuu huku taarifa zikionyesha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi hasa kaskazini Mashariki, Mashariki na eneo la Pwani.
"Mvua kubwa imesababisha barabara kukatwa katika maeneo na sehemu mbalimbali, hivyo kuvuruga mtiririko wa matumizi ya barabara kutokana na uharibifu wa barabara, na kufungia maji na kufanya baadhi ya barabara zisiweze kupitika," Murkomen alisema.
Zaidi ya watu 14 wamefariki Kaskazini mwa Kenya huku shirika la msalaba mwekundu nchini humo likisema zaidi ya watu 80,000 wamelazimika kuhama kufuatia mafuriko