Mvua endelevu ya muda mrefu inatarajiwa kudumu hadi Aprili mwaka ujao. Picha: Kenya Red Cross

Pembe ya Afrika imeshuhudia mvua kubwa inayohusiana na hali ya hewa ya El Nino ndani ya wiki za hivi karibuni.

Mvua hiyo imeua watu kadhaa, wakiwemo 46 sehemu mbalimbali nchini Kenya.

Aidha, Shirikisho la kimataifa la msalaba mwekundu limeeleza kuwa Kenya inakabiliwa na athari za El Niño, na kusababisha mafuriko katika kaunti 23 kati ya kaunti 47.

Naibu wa rais nchini humo Rigathi Gachagua amesema angalau nyumba 80,000 nchini Kenya zimeathirika "huku idadi ikizidi kuongezeka kila siku".

Ameongeza kuwa serikali inazidi kujitahidi "kuokoa watu wetu" ikiwa ni pamoja na uokoaji wa helikopta na huduma nyingine za dharura kutoa misaada na kuokoa familia zilizoathiriwa na mafuriko.

"Hali hii imeendelea kutishia maisha," alisema kwenye taarifa iliyotolewa Jumapili, akiwahimiza watu kuepuka maji ya mafuriko na kuhama kutoka maeneo ya chini.

Mvua endelevu ya muda mrefu inatarajiwa kudumu hadi Aprili mwaka ujao, aliongeza.

Wahusika walisema kuwa watu tisa wamefariki katika eneo la pwani tangu wiki iliyopita wakiwemo abiria wawili katika gari la mamlaka ya mapato Kenya KRA ambalo lilisombwa na daraja lililofurika maji katika kaunti ya Kwale Ijumaa asubuhi.

"Timu ya maafisa mbalimbali inayoongozwa na Huduma ya Ulinzi wa Pwani ya Kenya iko eneo la tukio ikijaribu kupata miili hiyo," Wizara ya mambo ya ndani ilisema Jumapili.

Shirika la reli Kenya, Kenya Railways, limesema mafuriko na maporomoko ya ardhi yamesababisha "ucheleweshaji usiotarajiwa" katika usafirishaji wa mizigo hadi bandari ya Mombasa na kwenye reli ya mizigo hadi Nairobi.

"Hii imeathiri shughuli za kawaida za treni, pamoja na uhamishaji wa mizigo, upakiaji na shughuli za upakuaji katika Bandari kuu ya Mombasa," shirika la reli linalomilikiwa na serikali ilisema katika taarifa Jumamosi iliyochapishwa kwenye X, zamani Twitter.

Shirika la Misaada la Uingereza Save The Children siku ya Alhamisi limesema kuwa, kutokana na mafuriko ya ghafla, zaidi ya watu 100 wakiwemo watoto 16 wamefariki dunia na zaidi ya 700,000 wamelazimishwa kutoka katika nyumba zao nchini Kenya, Somalia na Ethiopia.

Idadi ya watu waliohamishwa na mvua kubwa na mafuriko nchini Somalia "imeongezeka karibu mara mbili kwa wiki moja" hadi 649,000, shirika la umoja wa mataifa la misaada UNOCHA ilisema katika takwimu zake za hivi karibuni zilizotolewa Jumamosi.

AFP