Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imeunga mkono wito wa mataifa mbalimbali wenye azma ya kufanikisha amani Gaza huku mashambulizi ya Israeli dhidi ya Gaza yakiendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania January Makamba, kwa mahojiano ya kipekee na TRT Afrika, amesema kuwa Tanzania inaunga mkono upatikanaji wa suluhu ya kudumu ya mataifa mawili ya Palestina na Israeli.
"Watu wa Gaza wanastahili kupata haki zao kama binadamu wengine," Makamba amesema.
Aidha, Waziri huyo ameongeza kuwa serikali hiyo inaitisha usitishwaji wa mapigano yanayooendelea na kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadam bila masharti.
"Hali inayoendelea Gaza ni ya kusikitisha sana, na ni hali ambayo haipaswi kuendelea. Msaada wa kibinadam unatakiwa uwafikie kwa haraka bila masharti, na kutoa nafuu kwa watu kuanza upya maisha na kuendelea na maisha," Waziri Makamba amesema.
"Lazima kuwe na suluhu ya kudumu ambayo itahushisha mataifa mawili (two-State solution) ambayo yanaelewana na yana amani baina yao, huo ndio msimamo wetu sisi kama Tanzania," amemaliza.
Vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Gaza ambavyo vimeingia siku yake ya 198, vimewaua watu wasiopungua 34,097 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 76,980 tangu Oktoba 7, wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza imesema.