Rais wa Marekani Donald Trump amesema sera yake ni ya kurejesha Fahari kwa Marekani/ Picha: Reuters

Kama alivyoahidi mara kwa mara wakati wa kampeni za 2024, Rais Donald Trump alitoa msamaha mwishoni mwa Jumatatu kwa takriban watu 1,500 waliopatikana na hatia au kushtakiwa kwa jinai katika shambulio la Januari 6 kwenye Ikulu ya Marekani wakati Bunge la Congress lilipokutana kuthibitisha ushindi wa Biden wa 2020.

Trump pia amesimamisha utekelezaji wa sheria ya kupiga marufuku mtandao wa Tiktok.

"Ninamuamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali asichukue hatua yoyote kwa niaba ya Marekani kutekeleza Sheria kwa siku 75 kuanzia tarehe ya agizo hili, ili kuruhusu Uongozi wangu kupata fursa ya kuamua hatua inayofaa kuhusu TikTok," alisema katika amri yake.

Katika siku yake ya kwanza ofisini Rais Trump aliamuru Marekani ijiondoe katika mchakato wa dunia wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa atawasilisha mara moja taarifa rasmi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, au upande wowote husika, kuhusu kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano yoyote, mapatano au ahadi kama hiyo iliyotolewa chini ya Umoja wa Mataifa ya Mkataba wa Mfumo wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi," agizo lake lilisema.

Marekani inachangia pakubwa kifedha na rasilimali katika mchakato huo wa dunia wa kukumbana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Miaka ya hivi majuzi, Marekani imedai kujiunga na mikataba na mipango ya kimataifa ambayo haiakisi maadili ya nchi yetu au michango yetu katika kutekeleza malengo ya kiuchumi na kimazingira," Trump amesema.

"Makubaliano haya yanaelekeza dola za walipa kodi wa marekani kwa nchi ambazo hazihitaji, au hazistahili, usaidizi wa kifedha kwa maslahi ya watu wa Marekani."

Rais Trump pia amesema ataweka mikakati ya kupunguza mfufumko wa bei.

"Kwa hili ninaagiza wakuu wa idara zote za utendaji na mashirika kuwasilisha misaada ya bei ya dharura, kulingana na sheria inayotumika, kwa watu wa Marekani na kuongeza ustawi wa mfanyakazi wa Marekani," amesema.

"Hii itajumuisha kufuata hatua zinazofaa ili kupunguza gharama ya nyumba na kupanua usambazaji wa nyumba, kuondokana na gharama zisizo za lazima za utawala na mazoea ya kutafuta kodi ambayo huongeza gharama za huduma za afya, kuondoa mahitaji ambayo huongeza gharama za vifaa vya nyumbani, kuunda nafasi za ajira kwa wafanyakazi wa Amerika," yamesema maagizo ya Rais Trump.

Trump pia ameahidi kutetea haki ya watu wa Marekani.

"Hakuna afisa wa Serikali ya shirikisho, mfanyakazi, au wakala anayejihusisha na au kuwezesha mwenendo wowote ambao ungepunguza kinyume na katiba uhuru wa kujieleza wa raia yeyote wa Marekani," Trump amesema.

Uongozi wa Trump pia utalenga kukomesha mafuriko ya wageni haramu nchini Marekani.

Amesema Marekani itajenga ukuta na kuweka vikwazo vyengine dhidi ya wahamiaji kutoka Mexico.

Rais Donald Trump pia ameiondoa Marekani kutoka uanachama wa Shirika la Afya Dunaini, WHO.

TRT Afrika