Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale wakiwa na nakala za Makubaliano ya Ushirikiano wa Ulinzi huko Nairobi, Kenya. / Picha:  

Kenya na Marekani Jumatatu zilitia saini mfumo muhimu wa ushirikiano wa kiulinzi wakati wa ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani.

Mkataba huo muhimu unasisitiza ushirikiano wa kijeshi, unaimarisha ushirikiano wao katika mapambano dhidi ya makundi yenye itikadi kali kama vile al-Shabaab, na kufungua milango kwa Kenya kuongoza ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama nchini Haiti kwa msaada mkubwa wa Marekani.

Kenya mwezi Agosti iliahidi kupeleka kikosi cha polisi 1,000 waliofunzwa vyema ili kusaidia kurejesha hali ya utulivu na kupambana na ghasia za magenge ambayo yamekumba taifa hilo la Karibia.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin aliahidi msaada wa dola milioni 100 kwa ujumbe wa Haiti, akiangazia dhamira ya pamoja ya Marekani na Kenya katika kuleta amani, usalama na utulivu katika eneo hilo na duniani kote.

Muungano wa kimkakati

"Kutia saini mfumo wa ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi zetu mbili kunaimarisha umuhimu wa ushirikiano wetu wa kimkakati na Kenya," Austin alisema.

Aliongeza: "Itasaidia kuongeza uhusiano wetu wa ulinzi wa nchi mbili kwa miaka mitano ijayo."

Austin pia alitoa shukrani zake kwa Kenya kwa kuvikaribisha vikosi vya Marekani katika kisiwa cha Manda, pwani ya Kenya, akisisitiza umuhimu wa muungano wao wa kimkakati.

"Ushirikiano huu utatuwezesha kukabiliana vilivyo na changamoto za usalama zinazoendelea katika eneo letu na kwengineko."

Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale

Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale aliunga mkono maoni ya Austin, akielezea mkutano wao kuwa wenye tija kubwa.

Duale alipongeza kwa fahari kutiwa saini kwa mfumo wa ushirikiano wa ulinzi, ambao utadumu hadi 2028.

Alisema inawakilisha hatua muhimu katika uhusiano kati ya Kenya na Marekani na inasisitiza kujitolea kwao kwa pamoja kwa amani, usalama na utulivu katika kanda na kwengineko.

Duale alitaja maeneo matatu muhimu ya mijadala yao: kuthibitisha tena ushirikiano wao thabiti, kuimarisha ushirikiano wa kijeshi katika ulimwengu unaozidi kuwa mgumu licha ya kuunganishwa, na michango inayoendelea ya Kenya katika juhudi za kimataifa za kulinda amani.

"Ushirikiano huu utatuwezesha kukabiliana vilivyo na changamoto za usalama zinazoendelea katika eneo letu na kwengineko," Duale alisema.

Duale pia alisisitiza uwezekano wa ushirikiano katika nyanja ya teknolojia ya ulinzi na uvumbuzi, akisema kwamba mfumo huo hautaimarisha tu uwezo wa ulinzi wa Kenya lakini pia kuchangia ukuaji wa uchumi.

TRT Afrika