Wanajeshi wa Mali walikuwa wakiwapiga vita wanamgambo waliyokuwa mpaka wa Burkina Faso na Niger. / Picha: Reuters

Vikosi vya Mali vimemuua mmoja wa makamanda wakuu wa wanamgambo katika Sahel, jeshi lilitangaza Jumanne.

Abu Huzeifa, almaarufu Higgo, aliuawa Jumapili asubuhi wakati wa operesheni katika eneo la kaskazini la Menaka karibu na mpaka wa Niger, jeshi lilisema katika taarifa.

Aliwahi kuwa kamanda wa kijeshi wa kundi la kigaidi la Daesh/ISIS katika eneo la Sahel, katika eneo la mpakani mwa Mali-Niger-Burkina Faso.

Huzeifa anasemekana kushiriki katika shambulio la mwaka 2017 karibu na kijiji cha Tongo Tongo nchini Niger ambapo wanajeshi wanne wa kikosi maalumu cha Marekani na wanajeshi wanne wa Niger waliuawa.

Zawadi ya Marekani

Marekani hapo awali imeweka zawadi ya dola milioni 5 kwa yoyote atakayetoa taarifa ya mahali alipo.

Jeshi lilisema kuwa Huzeifa alikuwa raia wa kigeni, na ripoti zinaonyesha kuwa angeweza kutokea Sahrawi.

Kundi la Huzeifa liliripotiwa kufanya kazi katika eneo la Menaka nchini Mali, ambako lililaumiwa kwa mashambulizi kadhaa ya kigaidi dhidi ya raia wa Mali.

Burkina Faso, Mali na Niger zimepata hasara ya vifo vingi kutokana na ugaidi katika eneo hilo, kulingana na Global Terrorism Index 2024, ripoti iliyochapishwa na Taasisi yenye makao yake makuu Australia ya Uchumi na Amani.

Nchi hizo tatu zinakabiliwa na ongezeko la ukosefu wa usalama, huku makundi ya wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda na Daesh/ISIS yakihama kutoka Mali kuelekea nchi jirani katika eneo la Sahel.

TRT Afrika