Paul Makonda, Katibu Itikadi na Uenezi CCM. Picha/CCM

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Balozi Khamis Kagasheki ametahadharisha mwenendo unaotumiwa na katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala cha nchi hiyo CCM Paul Makonda wa kuwawajibishwa viongozi wa serikali hadharani.

Balozi Kagasheki ambae pia aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini na waziri wa maliasili katika serikali ya awamu ya nne, amesema kupitia mtandao wa X kwamba ni vyema kupata ufafanuzi wa utekelezaji wa serilaki lakini amesisitiza kwamba, hiyo isifanyike katika hali ya kudhalilisha viongozi.

"Zipo njia nyingi za kuhoji viongozi na kupata ufafanuzi kutoka kwao bila kuwavunjia heshima," amesema Kagasheki na kuongeza, “Duniani kote, serikali ni kioo cha nchi. Katika nchi za kidemokrasia vyama vya siasa hutafuta dola na kuunda serikali ambayo huwajibika kwa chama kile. Lakini style ya kutia kitimoto mawaziri na waziri mkuu na kuwapa ultimatum hadharani haijengi bali ina madhara.”

Paul Makonda katika moja ya ziara zake za hivi  karibuni katika Kanda ya Ziwa nchini Tanzania. Picha/CCM

Kagasheki ni miongoni mwa walioamua kuvunja ukimya na kukosoa mwenendo wa Paul Makonda, ambae hivi karibuni alichaguliwa na CCM kuwa Katibu wa Mwenezi na Itikadi wa chama hicho.

Makonda ni nani?

Jina la Paul Makonda sio geni katika masikio ya watu. Amekuwa gumzo kutokana na mambo kadhaa ambayo amekuwa akinasibishwa nayo na wakati mwengine mpaka kuwaacha watu vinywa wazi.

Hii ni kuanzia uteuzi wake kama mkuu wa wilaya wa Kinondonoi, Dar es Salaam, mwaka 2015 na aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, hatua iliyokosolewa na wale waliodai kuwa hakuwa na uzoefu wa kutosha.

Hata hivyo, akiwa DC, alipata umaarufu kwa mtindo wake wa kushughulikia matatizo ya jamii.

Baadae aliteuliwa kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na aliyekuwa rais wa Tanzania John Magufuli, Machi 2016.

Na alianza kazi mara moja, akiongoza operesheni kubwa dhidi ya uvutaji wa shisha jijini Dar es Salaam.

Mnamo mwaka 2017, Makonda alianzisha vita dhidi ya madawa ya kulevya kupitia mfululizo wa mikutano na waandishi wa habari iliyopeperushwa kupitia vyombo vya habari nchini humo ambapo aliwataja wanaoshukiwa kufanya biashara hizo, kuanzia wafanyabiashara, wanasiasa, viongozi wa dini, wasanii na baadhi ya raia wa kawaida.

Mwisho wake ulikuwa ni pale, alipojaribu kugombea ubunge wa jimbo la Kigamboni mwaka 2020, na kupoteza nafasi hiyo.

Jaribio hilo lilimtoa katika ulingo wa kisiasa na wengi walidhani pengine huo ndio ungekuwa mwisho wake.

Lakini hivi sasa anaonekana kurudi tena katika ramani ya siasa za nchi baada ya kuteuliwa CCM.

Ndani ya muda mfupi wa uteuzi wake, tayari amekuwa gumzo kutokana na maagizo yake.

Maagizo yaibua mjadala wa kisheria

Peter Madeleka, ambae ni wakili nchini humo anahoja mamlaka ya kisheria aliyokuwa nayo Makonda. “Anatakiwa awaombe radhi Watanzania hakuwa na hayo mamlaka ya kutoa maagizo yoyote yale kwa kiongozi yeyote yule wa serikali,” amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania.

Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa tetesi kwamba, uteuzi wake umeleta mpasuko ndani ya chama, baadhi bado wanaonyeshwa kufurahishwa na uteuzi wa Makonda huku wakimuona kama ni mwanasiasa safi mwenye safari ndefu ya mafanikio.

Kwa upande wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanahisi, kurudishwa kwake ni kwa kimkakati zaidi, hasa kipindi hiki ambacho tayari kuna vuguvugu ya kuelekea uchaguzi wa serikali za mtaa mwakani, na hatimae uchaguzi mkuu mwaka 2025.

TRT Afrika