Baada ya Rais Ruto kusaini muswada huo wa Tume ya IEBC kuwa sheria, atateua wanachama tisa wa jopo la uteuzi/ Picha Ikulu Kenya 

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kenya imeanza mchakato wa kuunda Tume ya Uchaguzi baada ya rais wa nchi hiyo William Ruto kusaini muswada wa kuundwa upya kwa Tume hiyo. Sheria hiyo mpya imekuja na marekebisho kadhaa yenye nia ya kuleta ufanisi zaidi katika uwazi na ufanisi zaidi wa Tume hiyo.

Kundwa upya kwa Tume hiyo kunafuatia kustaafu kwa waliokuwa makamishna wa IEBC akiwemo Mwenyekiti wake Wafula Chebukati aliyehudumu kwa miaka sita.

Viongozi hao kwa pamoja walistaafu 2023 baada ya kuratibu uchaguzi mkuu ambayo ulimuweka Rais William Ruto madarakani.

Kuzinduliwa upya kwa Tume ya IEBC inamaanisha kuwa Kenya sasa ina uwezo wa kuratibu uchaguzi wa aina yoyote.

Hata hivyo, baada ya Rais Ruto kusaini kuwa sheria, atateua wajumbe tisa wa jopo la uteuzi, mchakato ambao pia utapelekea kuteuliwa kwa mwenyekiti na makamishna wa Tume.

Kati ya majukumu ya Tume ya IEBC ni kusajili wapiga kura / Picha: AFP 

Wateuzi hawa watachangiwa na Tume ya Huduma za Bunge, Chama cha Wanasheria nchini, Baraza la Dini mbalimbali la Kenya na kamati ya uhusiano ya vyama vya siasa.

Ndani ya siku saba za uteuzi, jopo litatoa taarifa ya kuwataka wananchi kuanza kuwasilisha maombi ya kazi kwa wenye sifa, na hatimae kuchapisha orodha ya majina ya wenye sifa zao kwa ajili ya usaili.

Ndani ya siku 90, jopo hilo litachagua watu wawili waliohitimu katika nafasi ya uenyekiti na tisa kwa majukumu ya makamishna.

Kisha majina hayo yatawasilishwa kwa Rais, ambaye atamteua mtu mmoja kuwa mwenyekiti na sita kuwa makamishna.

Kuundwa upya kwa Tume ni utekelezaji wa mahitaji ya Gen Z kwa Rais William Ruto alipofanya majadiliano nao katika mtadao wa X Julai 5, 2024.

Vijana wa Gen Z wanaamini kwamba, kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi ni hatua muhimu itakayoweza kuwaondoa baadhi ya wabunge ambao wanadai hawafanyi kazi ipasavyo.

Kundwa upya kwa tume hii inakuja kufuatia kustaafu kwa waliokuwa makamishna wa IEBC akiwemo Mwenyekiti wake Wafula Chebukati aliyehudumu kwa miaka sita/ Picha AFP 

Changamoto za Tume zilizopita

Mitandaoni, tayari Wakenya wameanza kujadili ni nani atakaechaguliwa kushika nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi?

Tume za hapo awali zimekuwa na changamoto hasa baada ya uchaguzi mkuu zikilaumiwa kwa kuwa na upendeleo.

Changamoto kwa Tume ya Uchaguzi Kenya zilipamba moto zaidi 2007 wakati Tume ilipomtangaza hayati rais Mwai Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu ambao ulikosolewa na upinzani kwa madai ya kumpendelea Kibaki na hatimae kuibuka kwa vita vya kikabila nchini humo.

Machi 2013, Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Rais Uhuru Kenyatta kama mshindi lakini chama cha upinzani kilichoongozwa na Raila Odinga kiliikashifu hatua hiyo kwa madai kwamba, Tume ilitoa matokeo ambayo hayakuwa sahihi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Kiongozi wa Muungano wa Upinzani Azimio, Raila Odinga na vyama vyengine vya upinzania wamehusishwa katika kufanya marekebisho ya sheria ya Tume ya IEBC / Picha: wengine 

Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Uhuru Kenyatta mshindi wa urais lakini mahakama ya Juu nchini Kenya ilisema ushindi huo ulikuwa ni batili na kuamuru uchaguzi mpya kurudiwa ndani ya siku 60.

Agosti 2022, Tume ya Uchaguzi IEBC, ilimtangaza William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu lakini upinzani ukapinga na kusema Tume hiyo ilimpendelea Ruto na wakaipeleka Tume hiyo mahakamani.

Mahakama hata hivyo, iliamua kuwa ushindi wa Rais Ruto ulikuwa wa haki.

Lakini sasa, katika sheria hii mpya ya Tume ya IEBC 2024 ambayo rais Ruto ameipitisha, vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa vikiilalamikia Tume ya Uchaguzi vilipewa kipaumbele kuchangia marekebisho ambayo yataifanya Tume kuwa bora zaidi.

Wakenya wengi wanangoja kuona je, ni kina nani watachukua nafasi ya uongozi wa tume hiyo na iwapo utendaji wake utakuwa salama na malalamiko ya upinzani?

TRT Afrika