Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Felix Tshisekedi aliapa Jumatano (Januari 29) "kuchukua hatua kali na iliyoratibiwa" ili kudhibiti tena eneo lililotekwa na waasi wa M23, ambao waliteka mji wa mashariki wa Goma mapema wiki hii.
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Tshisekedi aliishutumu Rwanda kwa kuunga mkono uasi wa M23, akielezea matendo yao kama "biashara ya kigaidi" katika ardhi ya DRC,
"Wanajeshi wa Rwanda kuunga mkono kibaraka wao wa M23, ni kuendeleza harakati zao za kigaidi katika eneo letu, na kuzusha hofu miongoni mwa watu wetu," Rais Tshisekedi alisema,
Rwanda imekuwa ikikana kuunga mkono M23.
Aliwahakikishia wananchi wake pia anatambua maumivu na kero wanayopitia kutokana na mashambulizi haya.
" Vitendo hivi si shambulio kwa nchi pekee , lakini ni dharau kwa historia na utu wa watu wetu katika nyakati hizi ngumu, natoa wito kwenu kuwa na ujasiri na, zaidi ya yote, kupinga mambo haya," Tshisekedi aliongeza katika hotuba yake.
Rais Tshiskedi alisema ameitisha mikutano ya dharura na maafisa wa serikali na wanajeshi ili kutathmini hali ilivyo na kupanga hatua za kukabiliana nazo.
" Majeshi yetu ni mashujaa yenye silaha ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alama za ujasiri na uzalendo, yamehamasishwa kikamilifu, tayari kulinda kila sehemu ya eneo letu,: alihakikishia raia wa DRC.
Alizungumza katika hotuba yake wakati vikosi vya M23 vinaripotiwa kuelekea Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini, na kuzusha hofu ya kuongezeka kwa mzozo katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC.
"Tumechukua hatua muhimu za kidiplomasia, hasa ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na vile vile katika mchakato wa amani wa Luanda, ambao bado tunajitolea kikamilifu licha ya vikwazo. Tunapendelea njia ya mazungumzo, lakini kama kawaida, tuko imara, " Rais Tshisekedi amesema.