Treni ya Ethio-Djibouti, ambayo ilitimiza miaka mitano tangu uzinduzi wake mapema mwaka huu, ilifunga safari yake ya kwanza ya ujumuishaji wa kikanda kwa kupitia vituo kadhaa kuanzia Djibouti hadi Ethiopia huku ikielekea kituo chake cha mwisho cha jiji kuu la Addis Ababa, Ethiopia.
Msafara huo wa treni ya IGAD ni mojawapo ya mipango ya kuimarisha uhusiano kati ya raia wa nchi mbalimbali na mataifa, kuinua mwingiliano wa kitamaduni, kuboresha utalii, kuongeza uhamiaji wa wafanyakazi, kuinua uhusiano wa kibiashara, na kurahisisha safari za watu kati ya mataifa ya Afrika Mashariki.
Akiongoza uzinduzi huo katika kituo cha reli cha Nagad nchini Djibouti siku ya Jumapili, Katibu Mtendaji wa IGAD Dkt. Workneh Gebeyehu alisifia hatua hiyo kama njia ya kukuza ushirikiano wa mipaka kutokana na kuwepo na ukuaji wa njia za reli.
"Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, unaojulikana kwa ushirikiano wa kibiashara na uhamaji, ni mfano muhimu wa mshikamano wa kikanda na unafungua njia ya ushirikiano zaidi wa kikanda ili tuweze kutambua mustakabali ulio na ustawi, uelewano na ushirikiano baina ya mipaka." Alisema Dkt. Workneh.
Abiria kwenye treni hiyo walipata mapumziko Dire Dawa, na kusherehekea usiku wa kitamaduni, kabla ya kufuatiwa na sherehe ya upandaji wa miti katika Hifadhi kabla ya kuendelea na safari hadi Adama mjini.
Njia hiyo ya reli inasifika kwa kuchangia ukuaji wa uchumi wa Ethiopia kwani imesafirisha asilimia 98 ya kahawa ya Ethiopia hadi soko la kimataifa.
Reli hiyo pia inaunganisha bandari ya Bahari Nyekundu ya Djibouti na mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa huku Ethiopia, taifa lisilokuwa na bandari, likitegemea bandari ya Djibouti kwa huduma zake za usafirishaji na uagizaji.
Reli ya umeme iliyojengwa na China inayovuka mipaka yenye urefu wa kilomita 756 imekuwa ikifanya shughuli za kibiashara zaidi za usafirishaji wa mizigo kati ya miji miwili ya Addis Ababa na Djibouti.
Nchi kadhaa wanachama wa IGAD zina njia za reli zilizokuwepo awali na msafara wa ushirikiano wa kikanda wa Ethio-Djibouti ni sehemu ya mpango kabambe wa kufanya ndoto ya njia ya reli inayowaunganisha wote kuwa ya mafanikio.