Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amekutana na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed/  Picha PMO Ethiopia 

Kiongozi wa jeshi la Sudan amabaye pia ni kiongozi wa baraza la uongozi wa mpito Sudan jenerali Abdel Fattah al-Burhan amekutana na waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kiongozi huyo alifanya ziara rasmi kwenda Ethiopia Jumatano.

Tangu Aprili 2023 , Sudan imekuwa katika vita, huku jeshi la taifa la Sudan likipigana na kikundi la Rapid Support Forces, RSF.

Ethiopia pamoja na Sudan ni wanachama wa mamlaka ya maendeleo , IGAD.

Mamlaka hii imechukua kipaumbele katika kutafuta suluhu kwa vita hivyo.

IGAD imeteua Ethiopia kuwa katika kamati ya nchi ambazo zinafaa kuendesha mfumo wa upatanishi nchini Sudan kwa ajili ya kumaliza vita hivyo.

Sudan na Ethiopia ni majirani na tayari athari ya vita vya Sudan vimeifikia Ethiopia hasa huku watu wakitoroka Sudan na kutafuta afueni Ethiopia,

"Zaidi ya watu 89,400 wamevuka mpaka na kuingia wa Ethiopia tangu kuanza kwa mzozo wa Sudan," Umoja wa Mataifa umesema.

Ziara wa jenerali al Burhan inakuja baada ya ziara yake Kenya ambapo alikutana na rais William Ruto na wakakubaliana kuwa kuna umuhimu wa kuharakisha suluhu ya vita nchini Sudan.

Uhusiano wa Sudan na Ethiopia ni gani?

Mbali na kuwa majirani Ethiopia na Sudan wamekuwa na mvutano wao,

Nchi hizo pia zina mzozo kuhusu bwawa ambalo Ethiopia linajenga katika mto Nile/ picha: AFP 

Kwanza kabisa nchi hizo mbili zina mzozo wa ardhi katika eneo moja wa mipaka.

Nchi hizi zimezozana kwa miongo kadhaa katika eneo la mpakani la al-Fashaga lenye ukubwa wa kilomita za mraba 260, eneo ambalo WaEthiopia wanaliita Mazega.

Khartoum inasisitiza kuwa eneo hilo, ambalo linazunguka mpaka wa mashariki wa jimbo la Gedaref la Sudan na mipaka ya magharibi ya mikoa ya Amhara na Tigray ya Ethiopia, ni mali ya Sudan kwa mujibu wa ramani za enzi za ukoloni zilizochorwa zaidi ya karne moja iliyopita.

Mwaka wa 2007, viongozi wa nchi hizo mbili Omar al-Bashir wa Sudan na waziri mkuu Meles Zenawi walikubaliana juu ya utaratibu wa ushirikiano ambao raia wa Ethiopia na Sudan wangeweza kulima ardhi hiyo, na pande hizo mbili zilikubali kufanya kazi rasmi.

Lakini mabadiliko ya uongozi na misukosuko ya kisiasa katika nchi zote mbili imezidisha ushindani wa zamani kati ya majirani hao wawili na kurudisha mzozo wa al-Fashaga.

Nchi hizo pia zina mzozo kuhusu bwawa ambalo Ethiopia linajenga katika mto Nile. Great Ethiopian Renaissance Dam ina uwezo wa kuzalisha megawati 6000 ya nishati ikikamilika,

Misri na Sudan zimekuwa zikipinga Ethiopia kujenga bwawa hilo wakidai kuwa itapunguza maji ambayo yanatirikia kwenda nchini mwao.

Ethiopia imekuwa ikisisitiza kuwa bwawa hili litasaidia kupunguza mafurikoambayo hutokea mara kwa mara nchini Sudan.

Misri na Sudan zimeitaka Ethiopia kufuata maazimio ya nchi hizo mbili na Uingereza yaliyofanya miaka ya 1929 na 1959.

Makubaliano haya yalizipa nchi hizo mbili kipaumbele kwa maswala ya mto Nile.

Lakini Ethiopia imekataa maazamio hayo ikisema ni makubaliano ya wakati wa ukoloni ambao umepitwa na wakati.

Ethiopia ambayo inaendelea kujenga bwawa hilo imesema nchi zote 11 ambazo zinamiliki mto Nile zina haki ya kutumia maji hayo kwa maendeleo ya wananchi wake.

TRT Afrika