Taarifa kutoka idara ya kuchunguza harakati za ardhi inasema kuwa tetemeko la nguvu ya 4.6 kwenye vipimo vya Ritcher liligonga nairobi na baadhi ya viunga vyake usiku wa Jumanne.
Tetemeko hilo lililotokea mwendo wa saa 8:34 usiku, lilidumu kwa takriban sekunde 30.
Taarifa za tetemeko hilo zilitoka maeneo mbalimbali yakiwemo Kitengela, Ruaka, na Westlands. Wakazi wa Isinya, Kaunti ya Kajiado pia walihisi mitetemeko hiyo, sawa na wale wa Kirinyaga, Kisii, Nyeri, na Murang’ miongoni mwa mikoa mingine.
Hakuna ripoti zozote za majeruhi wala uharibifu wa majengo.
Kulingana na Earthquake Monitor, tetemeko hilo lilikuwa tetemeko la ardhi lenye nguvu ya 4.6, lililotokea kilomita 87 (54 mi) kutoka Nairobi kwenye kina kifupi sana cha kilomita 10 (6 mi). Kina hiki kifupi kilizidisha athari ya tetemeko karibu na kitovu.
Idara hiyo ya 'Earthquake Monitor' ilisisitiza kuwa matetemeko hayo ya kina kifupi kwa kawaida huhisiwa kwa nguvu zaidi ikilinganishwa na ya kina zaidi ya ukubwa sawa.
Mamlaka ilisema inafuatilia hali hiyo kwa karibu huku wakaazi wakiendelea kuwa macho kufuatia milipuko hiyo isiyotarajiwa.
Sio mara ya Kwanza kwa Kenya kupata tetemeko la ardhi. Jumla ya matetemeko 29 ya ardhi yenye ukubwa wa nne au zaidi yamepiga ndani ya kilomita 300 kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Tetemeko baya zaidi kuwahi kukumba Afrika Mashariki ni 2005 katika Ziwa Tanganyika lenye uzito wa 6.8 katika Richter.