Nigeria Kano Dawanau grain market

Serikali ya Tanzania imetangaza kuweka mikakati ya kudhibiti biashara ya mazao ya nafaka hadi nchi za nje huku ikitaja uamuzi huo kama mojawapo ya taratibu za kuimarisha ukusanyaji wa ushuru nchini humo na kuwalinda wafanya biashara wa ndani.

Haya yanajiri huku wizara ya kilimo ya Tanzania ikisimamisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara wa Uganda wanaohusika kwenye usafirishaji wa nafaka kutoka Tanzania kuelekea Uganda.

Tukio hilo limesababisha malori 200 ya mchele na mahindi yaliyokuwa yakielekea Uganda kuzuiliwa kwenye mpaka wa Mutukula kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri wa kilimo wa Uganda Hussein Mohamed Bashe, amewataka wafanyabishara kutoka nchi za kigeni kutii taratibu zilizowekwa ili kufanikiwa kwenye uwekezaji wao.

“Tumeanza utaratibu wa kurasimisha shughuli za kilimo. Kilichozuiliwa na serikali ni ufanyaji biashara ya mazao kinyume na sheria. Haiwezekana kushiriki biashara ya mazao ya nafaka bila leseni ya biashara.” Alisema waziri.

“Wafanyibishara wa nchi za kigeni wanahitajika kuingia mkataba na makampuni ya kitanzania na kununua mazao kupitia kampuni hizo. Au, asajili kampuni ndani ya Tanzania kwa mujibu wa sheria.” Aliongeza.

Kwa upande mwingine, wawakilishi wa wafanyibishara wa mazao ya nafaka kutoka Uganda wameiomba serikali ya Tanzania kuwaachilia waendelee na safari yao kama njia ya kuimarisha biashara katika Afrika Mashariki.

Marufuku hiyo ya utoaji vibali ilianza kutekelezwa na Tanzania kuanzia mapema mwezi huu huku nchi hiyo ikifafanua kuwa hivi karibuni itatoa mfumo mpya wa biashara ya nafaka inayopelekwa nchi za nje.

TRT Afrika