Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa nchi yake imebaini uwepo wa mtu mmoja anayesadikiwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Marburg.
Samia, ambaye alikuwa akiimpa mrejesho wa hali ya mlipuko wa Marburg nchini Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus siku ya Januari 20, jijini Dodoma, alisema kuwa, imebainika kwamba watu 25 waliokuwa wanahofiwa kuambukizwa ugonjwa wa Marburg walikuwa wanasumbuliwa na maradhi mengine na sio Marburg.
"Naomba niihakikishie Jumuiya ya Kimataifa kwamba Tanzania ni eneo salama kwa ajili ya kufanyia biashara na shughuli nyingine," alisema Rais Samia wakati akiwa mwenyeji wa Ghebreyesus.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameipongeza WHO kwa hatua ya haraka ya ufuatiliaji wa mlipuko wa ugonjwa huo nchini Tanzania, akiendelea kusisitiza kuwa nchi yake itachukua hatua madhubuti za kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
Hii ni mara ya pili kwa virusi vya Marburg kuripotiwa nchini Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza, virusi hivyo viliripotiwa kutokea mwezi Machi mwaka 2023, mkoani Kagera.